Makubwa Haya : MVULANA WA MIAKA 16 AOA BIBI WA MIAKA 70
Mvulana mmoja nchini Indonesia amemuoa mwanamke ambaye amefikisha umri wa miaka 70.
Kisa hicho ambacho kimeenda kinyume na
utamaduni na sheria pia kiligunduliwa baada ya video ya harusi ya wawili
hao kuanza kusambaa mtandaoni.
Bwanaharusi ana miaka 16 na kirasmi bado
ni mtoto lakini maafisa wasimamizi wa kijiji waliruhusu harusi hiyo
ifanyike baada ya wawili hao kudaiwa kutishia kujiua.
Chini ya sheria za Indonesia, mwanamke anafaa kuza na angalau miaka 16 na mwanamume miaka 19 ndipo mtu aruhusiwe kufunga ndoa.
Vyombo vya habari nchini humo vinasema
urafiki kati ya wawili hao ulianza kunawiri mwanamke huyo alipoanza
kumtunza mvulana huyo alipoanza kuugua Malaria.
Chifu wa kijiji chao Kusini mwa Sumatra
Cik Ani aliambia shirika la habari la AFP kwamba "kwa kuwa mvulana huyo
bado hajafikisha umri wa utu uzima, tuliamua harusi hiyo ifanyike
faraghani."
Anasema pia kwamba harusi hiyo
iliyofanyika tarehe 2 Julai ilifanyika "kuzuia dhambi ya uzinzi" kati ya
mvulana huyo kwa jina Selamat, na mke wake sasa ambaye anatambuliwa kwa
jina Rohaya.
Taarifa zinasema Rohaya ana umri wa kati ya miaka 71 na 75.
Babake mvulana huyo anadaiwa kufariki dunia miaka kadha iliyopita na mamake aliolewa na mwanamume mwingine.
Rohaya naye hii ni ndoa yake ya tatu na ana watoto kadha kutoka kwa waume zake wawili wa awali, taarifa zinasema.
Yenni Izzi, mwanaharakati wa kituo cha
Women Crisis Centre mjini Palembang ambaye hupigana dhidi ya ndoa za
utotoni, aliambia BBC kwamba harusi hiyo ni ya ajabu sana.
"Mvulana huyo aliamua kuoa si kwa sababu
za kiuchumi au kimwili lakini kwa sababu anashughulikiwa na kupendwa na
mwanamke huyo," alisema.
"Hajakomaa vya kutosha, kwa hivyo
kuangaziwa hivyo na kupendwa hivyo anafikiri kwamba wao kuishi pamoja
ndio suluhu pekee. Na kuishi pamoja kwake ni kuoana."
Maafisa wa serikali wa kanda wameeleza wasiwasi kuhusu kisa hicho, lakini haijabainika iwapo watachukua hatua.
Waziri wa masuala ya kijamii wa
Indonesia Khofifah Indar Parawansa amenukuliwa na gazeti la Jakarta Post
akisema kwamba ni "vigumu kwao kuoana rasmi hata katika afisi ya
kiongozi wa kidini kwa sababu mvulana huyo bado hajatimiza umri wa kuwa
mtu mzima".
Gavana wa jimbo la Sumatra Kusini Alex
Noerdin ameambia Sriwijaya Post kwamba "si harusi ya kawaida kamwe. Kuna
tofauti kubwa sana kwa umri.
"Katika visa vingi, wasichana ndio
huolewa wakiwa wadogo. Lakini katika kisa hiki, ni mvulana aliyeolewa na
ajuza, siwezi kusema zaidi ya hapo."
Chanzo-BBC