Mahakama Yakataa Ombi la Kigogo wa Escrow Harbinder Singh Seth Kutibiwa Nje ya Nchi
Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu imekataa ombi la Mawakili wanaomtetea
mfanyabiashara Harbinder Singh Seth la kumruhusu mteja wao kwenda nje ya
nchi kutibiwa uvimbe uliopo tumboni na badala yake apatiwe tiba kwenye
hospitali ya Taifa Muhimbili.
Wakili
wa kujitegemea, Alex Balomi aliifahamisha Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu jana kuwa Harbinder Singh Sethi anaumwa, hali yake imeendelea
kubadilika na hii ni wiki ya nne sasa hawezi kupata usingizi.
Wakili
Balomi aliiambia mahakama hiyo kuwa Sethi anasumbuliwa na uvimbe
tumboni ambao unahitaji uangalizi wa karibu wa madaktari.
“Kutokana
na hali yake kuwa mbaya hii ni wiki ya nne sasa hawezi kupata usingizi
hivyo anahitaji ungalizi wa karibu wa madaktari na kwamba wamebahatika
kupata nyaraka kadhaa kutoka kwa daktari,” Balomi aliifahamisha mahakama.
Balomi aliongeza kuwa hata siku aliyokamatwa alikuwa akienda kwenye matibabu Afrika Kusini.
Mwendesha
Mashtaka Mwandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,
Leonard Swai alisema nyaraka ambazo Wakili Balomi anataka
kuziwasilisha mahakamani hapo kuhusiana na Sethi hazijakidhi vigezo vya
kisheria na kwamba alitegemea daktari ambaye anamtibu angefika
mahakamani kueleza hali halisi ya ugonjwa husika.
Kutokana
na hoja hizo, Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi alisema suala la
ugonjwa si la kufumbiwa macho, linapaswa kuchukuliwa kwa uzito na
kuelekeza magereza kufanya kila linalowezekana kuhakikisha hali ya
mshtakiwa huyo inabaki katika hali nzuri na inapobidi wawasiliane na
wataalam wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Kesi imeahirishwa hadi Julai 28, 2017 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.
Katika
kesi hiyo, Sethi na James Rugemalira wanakabiliwa na mashtaka 12 ya
uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu,
kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za
udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola 22,
198,544.60 sawa na Sh 309,461,300,158.27.