Mahakama Yaamuru Harbinder Singh Sethi Akatibiwe Muhimbili
Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru mshtakiwa, Harbinder Singh Sethi
apelekwe katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kwa ajili ya
kupata huduma ya matibabu.
Hakimu
Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi alitoa amri hiyo jana Ijumaa Julai 28 baada
ya Sethi kuieleza mahakama hiyo kuwa hali yake kiafya bado ni mbaya na
kwamba aliongea na Magereza ili aweze kupata tiba toka kwa daktari
wake, wakampeleka katika Hospitali ya Amana.
Amedai
kuwa kutokana na maradhi yanayomkabili kuhitaji mtaalam ameshindwa
kupata matibabu, hivyo ameomba asinyimwe haki ya kupata matibabu.
Baada
ya kutolewa maelezo hayo, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), Vitalis Peter alieleza kuwa ni kweli
mshtakiwa ameieleza mahakama kuhusu hali yake lakini hakuna nyaraka
zinazounga mkono kutoka kwa mtaalam kuelezea hali yake.
Amebainisha kwa kuwa kutibiwa ni haki yake na kuwa wapo madaktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Magereza.
Hakimu
Shaidi alisema kusiwekwe kikwazo chochote kuhusu afya ya mshtakiwa
hivyo aliamuru Magereza kumpeleka Muhimbili kwa ajili ya matibabu na
tarehe ijayo watoe taarifa kama amri aliyoitoa imetekelezwa.
Upelelezi
wa kesi hiyo hadi sasa haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi Agosti
3, 2017 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa
umekamilika ama la.
Awali,
Julai 14, 2017, wakili wa Sethi, Alexi Balomi aliifahamisha mahakama
kuwa Sethi anaumwa na hali yake imeendelea kuwa mbaya na alikuwa hawezi
kupata usingizi kwa wiki nne.
Wakili
Balomi aliiambia mahakama kuwa Sethi anasumbuliwa na uvimbe tumboni
wenye ukubwa kama puto ambao unahitaji uangalizi wa karibu wa madaktari
wataalam na kwamba anahitaji uangalizi wa karibu wa madaktari.
Katika
kesi hiyo, Sethi na James Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka 12 ya
uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kutoa
nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu,
kutakatisha fedha na kuisababishia Serikali hasara ya Sh 309 bilioni.