MADA USHIRIKIANO KATI YA IDARA YA MAENDELEO YA JAMII NA ASASI ZA KIRAIA KATIKA KUDUMISHA ULINZI NA KULETA AMANI 1.0.UTANGULIZI

Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Mkoani Mara Victor Kabuje akiwasilisha Taarifa katika Mkutano wa wadau Ngazi ya Wilaya katika utatuzi wa Migogoro na ujenzi wa Amani Mara-Kaskzini ulioandaliwa na Shirika la Search For Common Ground. 
MADA USHIRIKIANO KATI YA IDARA YA MAENDELEO YA JAMII NA ASASI ZA KIRAIA KATIKA KUDUMISHA ULINZI NA KULETA AMANI
1.0.UTANGULIZI

Wizara ya  Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto  imeweka utaratibu wa  kuratibu mashirika yasiyo ya kiserikali kwa sheria  ya mwaka 2002 ambayo imeweka utaratibu wa ufanyaji kazi wa mashirika yasiyo ya kiserikali kwa uhuru  ukizingatia sheria za nchi.Katika ngazi ya Halmashauri Mashirika yanawajibika kwa idara ya Maendeleo ya jamii katika utendaji wa kazi ambapo Afisa Maendeleo ya jamii (W) ni Msajiri Msaidizi.Ambaye anapaswa kujua kazi zinazofanywa na mashirika katika Wilaya yake kuyaratibu kwa karibu na kuhakikisha hayakiuki Miongozo yao, katiba zao pamoja na sheria ya uanzishwaji wa mashirika yasiyo ya Kiserikali.NGO.

2.0.USHIRIKIANO KATI YA IDARA YA MAENDELEO YA JAMII NA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI.

Kama nilivyoeleza hapo juu upo ushirikiano kati ya idara na Mashirika yasiyo ya Kiserikali katika utendaji kazi kwa kudumisha ulinzi na usalama na kuleta amani.Maeneo ya ushirikiano ni:-

1)  Idara na Mashirika wamekuwa na ushirikiano katika kutekeleza shughuli mbalimbali zinazohusiana na masuala ya kijamii na kiuchumi ambayo yamekuwa yanapangwa na Mashirika au serikali.Hali inayosaidia kuwa na uwajibikaji wa pamoja.
 
2)  Mashirika yanapohitaji kutekeleza shughuli zake katika mamlaka za serikali za mitaa  huhitaji kupata utambulisho kutoka ngazi ya Wilaya ili kuondoa migongano kati ya NGOs na NGOs na wadau wengine wa Maendeleo ambao wanatekeleza miradi katika ngazi ya kata na Vijiji.

3)  Rasilimali zinazopatikana hutumika kwa pamoja kati ya Halmashauri na mashirika katika kuwaletea wananchi maendeleo hasa kwa asasi zilizowazi katika utendaji wake ambazo hazina vificho, hata hivyo yapo Mashirika yasiyo ya kiserikali ya kitapeli ambayo ni ya mfukoni kazi zao hazijulikani kwa wadau wengine na yakibainika huwa Idara inatoa taarifa kwa Msajiri na hatua za kuyafungia huchukuliwa.

4)  Tafiti zinazofanywa na wadau  hao Serikali na Mashirika zimekuwa zinatumika katika kupanga shughuli za kuwaleta maendeleo wanajamii.

5)  Idara huwa inatoa uthibitisho kwa wafadhiri kuwahakikishia kama shirika lipo na linafanya kazi zake au ni la wajanja wajanja, Taarifa ya idara huchukuliwa kwa uzito na watoa fedha kwa NGOs.ambao huamua kuendelea kuwapa fedha au kusitisha au kupunguza.

3.0. USHIRIKIANO KATI YA IDARA NA MASHIRIKA KATIKA KUDUMISHA ULINZI NA KULETA AMANI

1.   Idara na mashirika yasiyo ya kiserikali yamekuwa yanafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha kuna kudumisha ulinzi na kuleta amani kwa kutoa mafunzo mbalimbali katika jamii kwa kuhamasisha ulinzi na usalama na kuhakikisha jamii haijichukulii  hatua mkononi, elimu hutolewa kupitia mikutano ya hadhara.

2.   Pia ushirikiano upo katika kuwezesha mikutano ya viongozi wa mila ambao wamekuwa na umuhimu sana katika jamii kuhakikisha wanaondoa mapigano ya koo kwa koo yanayoleta  uvunjifu wa amani.Lakini pia Elimu hutolewa kwao kuwaelewesha umuhimu wa kuishi kindugu na kuachana na magomvi yasiyo na maana katika jamii.

3.   Elimu pia hutolewa kwa Idara kwa kushirikiana na Mashirika kwa jamii inayozunguka mgodi wa North mara juu ya kujiepusha na uvamizi wa mgodi kwa nguvu na kuwashauri kuwa na miradi mbadala na kuacha kutegemea uchimbaji tu,japo kumekuwa na ugumu katika hili kutokana na wakazi wa maeneo hayo kudai historia inawafanya iwe ngumu kufanya shughuli zingine,elimu itaendelea kutolewa.. 

4.   Idara na Mashirika yasiyo ya kiserikali wamekuwa wanabadilishana takwimu na taarifa mbalimbali ambazo ni muhimu sana kwa kila upande katika utekelezaji majukumu yake na kuhakikisha kunakuwa na amani katika Jamii na maendeleo endelevu.

5.   Idara imekuwa inashirikiana pia na mashirika yasiyo ya kiserikali na Jeshi la polisi na vyombo vingine vya kiusalama katika shughuli zake za kuleta maendeleo hasa kwa maeneo yanayohusika na uvunjifu wa amani katika jamii,mfano masuala ya ubakaji,ndoa za utotoni, unyanyasaji wa kijinsia na masuala ya ukeketaji wa watoto wa kike ambayo yanapelekea uvunjifu wa amani katika jamii.

4.0. MIKAKATI ILIYOPO KUHAKIKISHA KUDUMISHA ULINZI NA KULETA AMANI

1.   Vikao vya mara kwa mara kwa wadau wanaohusika ili kuondoa yale yanayoweza kupelekea uvunjifu wa amani kwa idara, NGOs,ofisi ya DC na vyombo vya ulinzi na usalama kwa pamoja.
2.   Jamii ya maeneo husika kushirikishwa ipasavyo katika kutatua changamoto zinazojitokeza zenye suala la uvunjifu wa amani ambapo viongozi wa mila,serikali za vijiji, kata na Tarafa wawe na ukaribu katika kushughulikia.

3.   Wadau wote wawe tayari kutenga fedha na vitendea kazi katika kufikia jamii husika, asitegemewe mdau mmoja tu, kila upande uone unawajibika katika hili.

4.   Utengenezwe mfumo utakao rahisisha upatikanaji wa taarifa kwa wadau wote muhimu zinazohusiana na ulinzi na kuleta amani katika jamii.

5.0.      MAFANIKIO  YALIYOFIKIWA 

1.   Vikao na mikutano ya uhamasishaji na elimu inayotolewa na wadau imepunguza athali mbaya ambazo zingesababisha uvunjifu wa amani

2.   Uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Halmashauri imesaidia maeneo ya mgodi wanaozunguka kutegemea uchimbaji tu na kupunguza wavamizi,pia hata maeneo mengine vijana wameanza kuwa na njia mbadala za kujiajiri.

5.1.      CHANGAMOTO.

1.   Baadhi ya mashirika kutoona umuhimu wa nafasi ya Halmasahuri wanapofanya kazi zao katika jamii na huenda moja kwa moja vijijini kutekeleza shughuli zao bila Halmashauri kuwa na taarifa.

2.   Baadhi ya mashirika kutokuwa tayari kulipa ada ya mwaka wala kuandaa taarifa na kuziwasilisha kwa Mkurugenzi Mtendaji(W).

6.0.HITIMISHO

Kudumisha ulinzi na kuleta amani kunahitajika nguvu ya pamoja kati ya Idara,Mashirika ,serikali kuu na wadau wengine Muhimu ikiwa ni pamoja na wananchi katika maeneo yao wanayoishi.

Victor Z.Kabuje
AFISA MAENDELEO YAJAMII (W)
TARIME



Powered by Blogger.