Kikwete amfariji Dk Mwakyembe...."Kifo Tumeumbiwa Sote"
Rais
wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ni miongoni mwa
waombolezaji wa kifo cha Linah, mke wa Waziri wa Habari, Sanaa,
Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kilichotokea juzi.
Kikwete amewasili msibani leo, Julai 17 saa sita mchana na kuweka saini kwenye kitabu cha maombolezo.
Kikwete amemfariji Dk Mwakyembe na kumtaka awe mvumilivu katika kipindi hiki kigumu.
"Mwakyembe
ni rafiki yangu wa siku nyingi, hata wakati mama anaumwa aliniambia na
nilienda kumjulia hali alipokuwa Muhimbili, nimtake awe mvumilivu
tunajua ana majonzi msiba huu ni wetu sote," amesema.
Wengine waliofika kumfariji Dk Mwakyembe ni Jaji Mstaafu Damian Lubuva, ambaye pia alimjulia hali Linah wakati akiwa hospitali.
"Nimekuja
kumpa pole Harrison, tunafahamiana muda mrefu na mkewe alipokuwa
anaugua pale Muhimbili nilikuwa naenda kumtembelea lakini juzi
nilivyokuwa kijijini ndiyo nimepata taarifa za mama yetu ametutoka. Ni
msiba wetu sote tunaelewa majonzi yake, uchungu aliyokuwa nao yeye na
familia yake lakini kifo kimeumbwa na Mwenyezi Mungu kinapotokea sote ni
tunatakiwa tumshukuru Mwenyezi Mungu," amesema.
Wengine
waliofika kumfariji Dk Mwakyembe ni Spika wa Bunge mstaafu, Anne
Makinda; Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji; Waziri wa
Ulinzi, Dk Hussein Mwinyi; Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga
na viongozi wengine wa Serikali waliopo madarakani na wastaafu.
Mjumbe
wa kamati ya mazishi, Andrew Magombano amesema mwili wa Linah utaagwa
kesho baada ya ibada itakayofanyika kwenye Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kunduchi kuanzia saa nne asubuhi.
"Baada ya ibada tutaaga na saa saba kamili tutaelekea uwanja wa ndege tayari kwa safari ya kwenda Mbeya," amesema Magombano.