HOTUBA YA MKUU WA MKOA WA SHINYANGA ZAINABU TELACK KWENYE KIKAO CHAKE NA WAWEKEZAJI NA WAFANYABIASHARA WA MKOA WA SHINYANGA
Mkuu
wa mkoa wa Shinyanga,Zainab Telack akizungumza na wafanyabiashara na
wawekezaji mkoa wa Shinyanga leo Alhamis Julai 20,2017-Picha na Kadama
Malunde-Malunde1 blog
HOTUBA
YA MHE. ZAINAB R. TELACK, MKUU WA MKOA WA SHINYANGA KWENYE KIKAO CHAKE
PAMOJA NA WAFANYABIASHARA WA MKOA WA SHINYANGA TAREHE 20/07/2017.
Mwenyekiti wa TCCIA,
Katibu Tawala Mkoa,
Wahe. Wakuu wa Wilaya,
Wakuu wa Sehemu na Vitengo, Sekretarieti ya Mkoa,
Wakurugenzi na Mameneja wa Mamlaka na Taasisi za Serikali,
Wawekezaji na Wafanya Biashara,
Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana.
Habari za asubuhi.
Awali
ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa wema
wake kuendelea kutulinda, hatimaye kuweza kukutana siku ya leo.
Ndugu washiriki
Nimewaiteni
kwa nia ya kuja kuwafahamisha umuhimu wenu katika kuchochea maendeleo
ya kiuchumi katika Mkoa wetu na Taifa kwa ujumla, kuwaomba tudumishe
mahusiano kati yetu – Serikali na ninyi Sekta Binafsi ili kila upande
uweze kunufaika kama ilivyokusudiwa.
Lakini
pia nimewaiteni ili niweze kuwafamisha kuwa huu ni mwaka wa pili wa
utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano (2016/17 –
2020/2021) wenye dhima ya ‘‘Kujenga Uchumi wa Viwanda ili Kuchochea Mageuzi ya Maendeleo ya Watu’’.
Ili
kutimiza malengo ya Mpango huu ni lazima Serikali ifanye kazi kwa
ushirikiano wa karibu sana na Sekta Binafsi, na ninyi ni sehemu ya Sekta
Binafsi. Ili kudumisha ushirikiano huo Serikali imeanzisha Mabaraza ya Biashara katika ngazi za Taifa, Mikoa na Wilaya.
Mabaraza
haya yanaundwa jumla ya wajimbe 40 kwa uwiano sawa kati ya Sekta ya
Umma na Sekta Binafsi, yaani wajumbe 20 kutoka Sekta ya Umma na wajumbe
20 kutoka Sekta Binafsi.
Na
baadhi yenu ni wajumbe wa mabaraza haya. Madhumini ya mabaraza haya ni
kutengeneza mazingira bora ya kufanya biashara na uwekezaji, kuibua
fursa za uwekezaji na kuzinadi fursa hizo kupitia vikao, mikutano,
makongamano, majukwaa na midahalo ya uwekezaji.
Nitumie
fursa hii kuwasihi wajumbe wa Baraza la Biashara la Mkoa mliopo sasa na
mtakaoteuliwa kwa nyakati za baadaye kushiriki kikamilifu vikao,
mikutano, makongamano, majukwaa na midahalo ya uwekezaji kila
mnapohitajika, ili muweze kutumia vizuri nafasi mliyopewa; kwani mmepewa
dhamana ya kuwakilisha kundi kubwa la wawekezaji na wafanyabiashara
wenzenu.
Napenda
kutumia fursa hii kuwaandaa kwa ajili ya kushiriki kwenye Jukwaa la
Uwekezaji litakalofanyika hivi karibuni katika Mkoa wetu; kupitia Jukwaa
hilo Mkoa utapata nafasi ya kutangaza fursa zake za uwekezaji kwa wadau
walio ndani na nje ya nchi.
Lakini pia wafanya biashara na wenye viwanda watapata nafasi ya kutangaza bidhaa zao ndani na nje ya nchi.
Ndugu washiriki
Uwekezaji
ni moja ya shughuli zinazochochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa
Shinyanga na Taifa kwa ujumla. Hadi sasa Mkoa una jumla ya viwanda 81;
ambapo viwanda vikubwa ni 18, viwanda vya kati ni 9 na viwanda vidogo ni
54.
Napenda
kuchukua fursa hii kuwapongeza wafanya biashara na wawekezaji wote
kutoka ndani na nje ya nchi kwa mchango wenu mkubwa katika uwekezaji,
utoaji wa ajira kupitia biashara na viwanda vyenu na mchango wenu katika
ukuaji wa uchumi na mapato ya ndani kupitia malipo ya kodi.
Ikumbukwe
kuwa kwa sehemu kubwa jukumu la uwekezaji linatekelezwa na sekta
binafsi; kazi ya Serikali ni kuandaa mazingira rafiki kwa ajili ya
wawekezaji kama vile kudumisha amani na utulivu, kuweka miundombinu ya
maji, barabara, reli, umeme wenye uhakika na upatikanaji wa nishati
mbadala kwa gharama nafuu.
Kazi
nyingine ya Serikali ni kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji na kuweka
mazingira mazuri kwa ajili ya uzalishaji na upatikanaji endelevu wa
malighafi inayohitajika kwenye viwanda. Vitu hivi vikikosekana hakuna
uwekezaji utakaofanikiwa kwa namna yoyote mahali popote.
Ndugu Washiriki
Mkoa
wa Shinyanga umetenga jumla ya Hekta 22,099.12 kwa ajili ya uwekezaji
wa miundombinu ya biashara, kilimo na viwanda kama ifuatavyo:-
Halmashauri ya Mji wa Kahama imetenga Hekta 2,000, Halmashauri ya Wilaya
ya Shinyanga Hekta 5,560, Ushetu Hekta 2,110, Kishapu Hekta 10,361.70,
Manispaa ya Shinyanga Hekta 1,809.87 na Msalala Hekta. 257.53.
Kufuatia
uhamasishaji unaoendelea kufanywa na Mkoa, viwanda vingi vya kuchakata
mazao ya kilimo na vimeanzishwa na kusababisha mahitaji makubwa ya
malighafi kama vile pamba, mbegu za alizeti, matunda ya maembe na
mapera, maharage ya soya, mpunga pamoja na pumba zake.
Kufuatia
hali, naomba kutumia fursa hii kuwahamasisha kuwekeza katika kilimo cha
kisasa cha umwagiliaji kwa lengo la kupata mavuno yatakayotosheleza
mahitaji ya viwanda vyetu; kwani soko la mazao mtakayozalisha ni la
uhakika kutokana na uwepo wa viwanda vya kuchakata malighafi husika.
Fursa
zingine za uwekezaji katika Mkoa wetu ni pamoja na ujenzi wa viwanda
vya nguo, nyama, ngozi na bidhaa zake. Fursa zingine ni kuwekeza katika
viwanda vya kuongeza thamani madini ya dhahabu.
Ndugu washiriki
Suala
la hifadhi ya mazingira ni muhumi kwa nchi yoyote yenye maono endelevu
ya kuimarisha sekta ya viwanda na ustawi wa jamii yake.
Viwanda
vinapoendeshwa bila kuzingatia hifadhi ya mazingira vinakuwa ni chanzo
kikubwa cha uchafuzi wa mazingira, hali inayopelekea athari mbalimbali
katika jamii kama vile milipuko ya magonjwa, mabadiliko ya tabia nchi,
ukame, kuongezeka kwa joto kwenye uso wa Dunia na mvua kubwa kupita
kiasi inayopelekea kutokea kwa mafuriko.
Serikali
inatambua hilo na ndiyo maana katika Maadhimisho ya Siku ya Mazingira
Duniani yaliyofanyika Kimkoa Wilayani Kishapu mwaka huu Kaulimbiu
ilikuwa ‘‘Hifadhi ya Mazingira Mhimili kwa Tanzania ya Viwanda’’.
Mazingira ya Mkoa wa Shinyanga yamekuwa kivutio kikubwa cha wawekezaji wa ndani na nje ya Nchi.
Viwanda
vikubwa vimekuwa vikijengwa Mkoani tangu kukamilika kwa mradi mkubwa
wa maji ya Ziwa Victoria, uwepo wa umeme wa gridi ya Taifa, usafiri kwa
njia ya reli na barabara ya lami inayounganisha Mkoa wa Shinyanga na
Majiji makubwa ya Arusha, Mwanza na Dar es Salaam pamoja na nchi za
Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa
Congo, vimekuwa ni vivutio vikubwa vya uwekezaji.
Ndugu washiriki
Suala la kupata taarifa sahihi ni muhimu sana kama tunataka kuendesha shughuli zetu kwa ufanisi.
Taarifa zinapatikana kwa njia nyingi ikiwa ni pamoja na kupitia vyombo vya habari, mikutano na mitandao.
Njia
ya kupata taarifa kwa njia ya mikutano ni moja ya njia madhubuti kwani
unapata muda wa kubadilishana mawazo na uzoefu ana kwa ana, unapata muda
wa kuuliza na kujibiwa maswali yako kwa uhuru zaidi; ndiyo maana leo
tumeweza kuitana mbali na kufahamiana, lakini pia tutaweza kubadilishana
uzoefu katika uendeshaji wa biashara, pamoja na kujadili namna ya
kutatua changamoto zinazotukabili kwenye biashara zetu.
Napenda
kutumia fursa hii kuwashukuru kwa mara nyingine kwa kuitikia wito huu,
kwani kikao hiki ni dalili nzuri ya ushirikiano kati ya Serikali na
Sekta Binafsi.
Mikutano
kama hii ni muhimu kwani tunapata nafasi ya kupeana taarifa muhimu kama
vile fursa za uwekezaji zilizopo, upatikanaji wa masoko ya bidhaa zetu
na mbinu endelevu za kupata malighafi kwa ajili ya viwanda vyetu; yote
haya ni kwa nia ya kuhakikisha kuwa tunafikia malengo ya taasisi zetu na
Taifa kwa ujumla.
Baada
ya maelezo haya, napenda kutamka kuwa kikao hiki cha Wafanya Biashara
wa Mkoa wa Shinyanga, kimefunguliwa Rasmi leo Tarehe 20 Julai, 2017.
Nawatakieni kikao chema na majadiliano yenye mafanikio.
Asanteni kwa kunisikiliza.