HAWA NDIYO WAJUMBE WAPYA WA KAMATI YA UCHAGUZI TFF,BAADA YA WALE WA MWANZO KUCHINJWA
KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) imefanya mabadiliko ya Kamati ya Uchaguzi na kuwaengua
Wajumbe wanne walioonyesha kumtetea Rais wa shirikisho hilo, Jamal
Malinzi ambaye kwa sasa yuko rumande kwa tuhuma mbalimbali.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya kikao cha
Kamati ya Utendaji ya TFF kilichofanyika leo mchana makao makuu ya
shirikisho hilo, Uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam chini ya Kaimu
Rais, Wallace Karia.
Wajumbe walioondolewa ni pamoja na
Makamu Mwenyekiti, Wakili Domina Madeli, Juma Lallika, Jeremiah Wambura
na Hamim Mahmoud Omar na sasa Mwenyekiti, Wakili Revocatus Kuuli
atafanya kazi na Mbunge wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa, Wakili Malangwe
Ally Mchungahela, Wakili Kiomoni Kibamba ambaye pia ni Mkurugenzi wa
Jiji la Mwanza ma Wakili Thadeus Kalua.
Kabla ya hapo, Mwenyekiti Kuuli
alitofautiana na Wajumbe wenzake wote wa Kamati hiyo ya awali juu ya
Malinzi kuruhusiwa kuendelea kuogombea katika uchaguzi wa Agosti 12,
mwaka huu mjini Dodoma licha ya kwamba hakutokea kwenye usajili.
Mchakato wa uchaguzi wa TFF sasa utaendelea bila Jamal Malinzi (katikati)
Malinzi hakutokea kwenye usaili kutokana
na kuwa anashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU) kabla ya kufikishwa Mahakamani kusomewa mashitaka 28, ambayo
yalimfanya anyimwe dhamana na kupelekwa rumande hadi Julai 17, mwaka huu
upelelezi wa kesi uyake utakapokamilika.
Wakili Kuuli alipingana na wenzake
waliotaka Malinzi aruhusiwe kuendelea na mchakato japo hakushiriki
usaili na kufikia kuvunja kikao, kisha kupeleka taarifa Kamati ya
Utendaji ya TFF, ambayo nayo baada ya kikao chake cha leo imefikia
uamuzi wa kuiunda upya Kamati ya uchaguzi pamoja na Kamati nyingine.
Kamati nyingine zilizotajwa na Kaimu
Katibu Mkuu wa TFF, Salum Madadi leo ni Kamati Maadili ambayo inaindwa
na Mwenuekiti, Amidou Mbwezeleni, Steven Zangira, Mkuu wa Wilaya ya
Tarime mkoani Mara, Glorius Luoga, Walter Lungu na Amin Bakhresa.
Kamati ya Rufaa ya Maadili; Wakili
Rugemeleza Nshala, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, DCP Mohammed
Mpinga, Wakili Benjamin Karume, Dk Lisobine Chisongo, ASP Benedict
Nyagabona.
Kamati ya Nidhamu; Tarimba Abbas, Peter
Hela, Boniface Lyamwike, Dk Billy Aonga na Kassim Dau, Kamati ya Rufaa
ya Nidhamu; Wakili Rahim Zubeiry Shaaban, Siza Chenga, Abbas Mtemvu,
Amani Mulika na Stella Mwakingwe wakati Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi
inaundwa na Wakili Abdi Kagomba, Kenneth Mwenda, Rashid Sadallah, Jabir
Shekimweri na Mohamed Gombati.
Sasa Kamati mpya ya Uchaguzi inatarajiwa
kuendelea na mchakato, ambao ulisimamishwa kwa muda Julai 2 ukiwa
katika hatua ya usaili.
Malinzi, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine
Mwesigwa kwa pamoja na Mhasibu, Nsiande Isawafo Mwanga wako kwa
mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya TFF
iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam na wanatarajiwa
kufikishwa tena Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam Julai
17, mwaka huu.
Wakati huo huo: Ujumbe wa Shirikisho la
Soka la Kimataifa (FIFA) hautakuja tena nchini baada ya mazungumzo na
Kaimu Rais wa TFF, Wallace Karia kwa njia nya simu.
Karia amesema katika mazungumzo hayo
amewaeleza kila kitu kinachoendelea nchini ikiwemo kikao cha leo cha
Kamati ya Utendaji na wameridhika na kuitakia kila la heri kamati hiyo.
“FIFA hawatakuja tena, tuliongea nao
tukawaeleza kinachoendelea, walitupigia wakitaka kujua kama kulikuwa na
muingilio wa serikali katika mchakato, au kama kuna fedha za FIFA
zilizotumika vibaya, tukawaambia siyo kweli na kuwaeleza kilichotokea
kwa hiyo hawatakuja,” amesema Karia.