Naibu Waziri afanya ziara ya kushtukiza mradi wa umeme Kinyerezi II, atoa agizo
Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Medard Kalemani ameagiza Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) kuhakikisha mradi wa umeme wa Kinyerezi II unazalisha
megawati 30 za umeme nchini ifikapo Desemba mwaka huu.
Kalemani amefanya ziara ya kushtukiza katika mradi huo leo asubuhi (Juni 30) ili kujua hali ya utendaji.
Amesema
taarifa aliyopewa tangu alipowasili ni kuwa mradi huo utazalisha
megawati 240 utakapokamilika mwakani ila 30 zikamilike Desemba mwaka
huu.
"Mradi
wa Kinyerezi II tunategemea utupatie megawati 240, lakini lazima tuanze
kupata hizo mapema, kwa taarifa niliyosikia tutaanza na megawati 30
sasa niseme megawati hizo tupate ifikikapo Desemba," amesema Kalemani.
Amesisitiza kuwa zitakazobakia apewe ratiba za utekelezaji wake ili hadi kufikia Septemba 2017 megawati zote ziwe tayari.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Tanesco, Tito Mwinuka ameomba ushirikiano
baina ya Serikali na Shirika hilo ili kufika malengo ya agizo la Naibu
Waziri.
"Tushirikiane pamoja Tanesco na Serikali kuhakikisha fedha zinapatikana kwa wakati ili kwamba mradi ukamilike kwa wakati," amesema Mwinuka.
Kalemani
ameongeza kuwa hakutakuwa na uongezaji wa muda katika miradi yote
miwili ya Kinyerezi I na II hivyo kuwataka wahusika kufanya kazi kwa
nguvu na weledi ili kumaliza kazi.
Amesema
mradi wa Kinyerezi I umefikia asilimia 35 hali ambayo hairidhishi huku
ukitegemewa kutoa megawati 185 kufikia Agosti 2017.
"Kufikia
Septemba mwakani, tunategemea kuwa na megawati 425 kwa miradi yote
miwili bila kupungua, fanyeni kazi sana katika Kinyerezi I," amesema Kalemani.