Mawakili 248 waapishwa, Tundu Lissu awataka kutumia taaluma yao kusaidia jamii
Na Eliphace Marwa – Maelezo
Kaimu
Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Mawakili wapya
kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya taaluma ya uwakili na kutumia
taaluma zao kwa kutoa msaada wa kisheria kwa jamii.
Aliyasema
hayo jana Jijini Dar es Salaam wakati wa Sherehe za 56 ya kuwapokea na
kuwaapisha Mawakili wapya 248 iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama
Kuu jijini Dar es Salaam.
Aidha
Kaimu Jaji Mkuu aliwahimiza Mawakili wapya kujiendeleza kitaaluma kwa
sababu kuwa wakili sio mwisho wa taaluma kwani wanahitajika kusoma
sheria za nchi mbalimbali Duniani ili kuweza kuingia mikataba ya
kimataifa.
Alisema
mawakili wapya wanatakiwa washiriki katika kutoa haki, wawe waaminifu
kwa mahakama na wateja kwani wakienda kinyume haki itapotea.
“Mawakili
wote wanatakiwa kuwa waaminifu kwa wateja wanaowahudumia na
kushirikiana na mahakama katika kutoa haki na wasiwe mawakala wa rushwa
bali wawe mawakala wa kutenda haki,” alisema Kaimu Jaji Mkuu Prof. Ibrahim.
Aidha
Kaimu Jaji Mkuu aliwataka mawakili hao kufika maeneo ya nje ya mji ili
wasaidie upatikanaji wa haki kwani kumekuwa na changamoto kubwa ya
mawakili katika maeneo ya nje ya miji.
Naye
Rais wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS) Tundu Lissu aliwataka
Mawakili hao kutumia taaluma hiyo katika kuisaidia jamii kujua haki zao
na utawala wa sheria japo kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili
tasnia ya sheria nchini.
“Napenda
kuwatakia kila la kheri mawakili hawa wapya ila niwaombe watumie
taaluma hii kwa kuisaidia jamii kujua haki zao pamoja na utawala wa
sheria,” alisema Mh. Tundu Lissu.
Idadi ya mawakili walioapishwa jana imepelekea Tanzania kuwa na idadi ya zaidi ya mawakili 6300.