MICHUANO YA CONFEDERATION CUP NI YA WIKI MBILI TU, LAKINI ZAWADI ZAKE NI MABILIONI YA FEDHA, STARTIMES WAANZA KUIONYESHA LIVE
MEXICO
Na Saleh Ally
MOJA ya michuano mifupi ambayo imekuwa na burudani kubwa ni ile ya Kombe la Mabara, maarufu kama Confederation Cup.
Rasmi imeanza jana kwa wenyeji Russia kuwatwanga New Zealand kwa mabao 2-0 katika mechi ya ufunguzi. Mechi hiyo ilionyeshwa moja kwa moja kupitia king'amuzi cha StarTimes na mechi zijazo zitaendelea kuonyeshwa mubasharaa.
Michuano hii inakutanisha mabingwa wa mabara na pia utawaona mabingwa wa dunia na anayepatikana hujulikana ni mbabe wa wababe.
Watanzania wamekuwa wakiifuatilia michuano hii kwa kuwa mastaa wengi wanakuwa upande huu kwa kipindi hiki baada ya ligi zote maarufu kumalizika na mabingwa kupatikana.
Bahati kubwa kwa wapenda soka hapa nchini, michuano hiyo wataishuhudia kupitia King’amuzi cha StarTimes ambacho kimepata haki ya kuonyesha mechi zote za timu nane zinazoshiriki michuano hiyo.
Wakati watu wakiwa wanasubiri kuishuhudia michuano hiyo mubashara kupitia StarsTimes, tujadili suala la zawadi.
Wako ambao wamekuwa wakiamini michuano mikubwa kama hiyo huwa inafanyika kwa ajili ya heshima za timu au wachezaji kutaka kupata mafanikio na kuboresha rekodi walizonazo.
Huo unaweza kuwa upande mmoja lakini ukweli, wachezaji wamekuwa wakipambana pia kuhakikisha wanaweka heshima ya kubeba ubingwa lakini pia kufanikiwa kupata posho.
Michuano ya Kombe la Mabara ni ya wiki mbili tu, rasmi ikianza leo hadi Julai 2, lakini atakayeibuka na ubingwa, atabeba dola milioni 5 (zaidi ya Sh bilioni 11)
RUSSIA
Kuingia fainali tayari ni kujihakikishia kubeba dola milioni 4.5 (Sh bilioni 9.8) na dola milioni 3.5 (Sh bilioni 7.6) zitakwenda kwa mshindi wa tatu, mshindi wa nne au timu ya mwisho kuingia robo fainali itabeba dola milioni 3 sawa na Sh bilioni 6.5.
Kama haitoshi, nafasi ya tano hadi ya nane kila timu inalamba dola milioni 2 (Sh bilioni 4.3), hivyo kuifanya kuwa michuano yenye zawadi kubwa kutokana na muda wake mchache.
Ukiangalia jumla zawadi pekee kabla ya maandalizi ni kitika cha dola milioni 22 (Sh bilioni 48.2).
Upande wa maandalizi, Urusi ambao wataandaa Kombe la Dunia mwaka 2018, wanaonekana wamejiandaa kweli na wako sawa hasa.
Kuna makundi mawili yenye timu nne kila moja na viwanja vitakavyotumika ni vinne Otktytiye Arena ulio jijini Moscow na una uwezo wa kuchukua watazamaji 45,360, Uwanja wa Fisht Olympic uko jijini Sochi na unaochukua watazamaji 47,659.
Uwanja wa tatu ni Krestovky wa jijini Saint Petersburg, unabeba watazamaji 68,134 na ndiyo mkubwa zaidi kwa viwanja vitakavyotumika kwa michuano hiyo. Uwanja wa wanne ni Kazan Arena, watu 45, 379 ndiyo wanaingia na uko mjini Kazan.
Viwanja hivyo pia ni sehemu ya burudani kwa kuwa maandalizi yanayofanyika yanajenga mazingira ya kuwafanya mashabiki wa soka watakapokuwa Urusi wapate burudani hasa ya soka.
Ushindani lazima utakuwa mkubwa kwa kuwa wachezaji nyota kama Cristiano Ronaldo akiwa anaiongoza Ureno atataka kufanya makubwa zaidi baada ya kufanikiwa kubeba Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na Real Madrid, hivi karibuni.
Wakati Ureno ikiwa na Ronaldo lakini kumbuka kuna Chile inayoongozwa na Alexis Sanchez ambaye pia anaitaka nafasi hiyo kama ambavyo timu yenye wapiganaji wengi Cameroon ambao ni mabingwa Afrika wanavyotaka kubeba ubingwa huo na kubadilisha mambo.
Timu ya Afrika inaonekana iko katika mlima mrefu usioweza kuupanda lakini Cameroon wameapa kuwa kama walivyofanya kwenye Afcon na kushangaza wengi, wataendelea na ‘surprise’.
Usiwasahau mabingwa wa dunia, Ujerumani wakiongozwa na watu kama Mesut Ozil na Thomas Muller. Hii ni timu imara kabisa lakini lazima ifanye kazi ya ziada.
Mexico nao si wa kubeza kwa kuwa wameshiriki michuano hiyo mara nyingi zaidi kuliko timu nyingine zilizo katika michuano hiyo.
Mexico imeshiriki mara 6, inafuatiwa na New Zealand na Australia ambazo kila moja imeshiriki mara tatu.
Haitakuwa michuano rahisi inayoweza kutabirika. Wale watakaoishuhudia kupitia StarTimes watakuwa na jibu.
ZAWADI:
Nafasi ya 5 hadi 8, USD milioni 2 (zaidi ya Sh bilioni 4)
Mshindi wa nne USD milioni 3 (zaidi ya Sh bilioni 5)
Mshindi wa tatu USD milioni 3.5 (zaidi ya Sh bilioni 8)
Mshindi wa pili USD milioni 4.5 (zaidi ya Sh bilioni 10)
BINGWA USD milioni 5 (zaidi ya Sh bilioni 11)