Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) ambaye ni Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas.
WASIO na taaluma ya Utangazaji na
Uandishi wa Habari nchini, wanaofanya kazi kama watangazaji au waandishi
wa habari katika vyombo mbalimbali vya habari, wametakiwa kutumia vyema
miaka mitano waliyopewa kisheria kwa ajili ya kujiendeleza, ili kuepuka
kutotambuliwa katika tasnia ya habari baada ya muda huo kuisha.
Aidha, wametakiwa kutopoteza muda kupiga
kelele na kufanya mashauriano yasiyowasaidia kuhusu uamuzi huo wa
kisheria, kwa sababu kiwango cha chini cha elimu ya mwanahabari
kilichokwishaamuliwa kupitia Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016 ni
Stashahada ya Uandishi wa Habari na si uzoefu wa kuandika, ubunifu wala
sauti nzuri ya kutangaza pekee.
Ushauri huo ulitolewa na wadau
mbalimbali wa habari pamoja na wanazuoni Dar es Salaam jana, baada ya
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe,
kulieleza Bunge mjini Dodoma juzi kuwa asilimia 90 ya watangazaji nchini
hawana taaluma ya Utangazaji wala Uandishi wa Habari, hivyo kusababisha
weledi na maadili ya kazi hiyo kushuka.
Alisema hayo wakati akiwasilisha bajeti
ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2017/18. Mkurugenzi wa Idara ya Habari
(Maelezo) ambaye ni Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas, alisema
Sheria hiyo ya Huduma ya Habari imetoa fursa maalumu kwa watu wote wasio
na taaluma ya uandishi wa habari kwenda shule kujiendeleza kufikia
angalau kiwango cha chini cha elimu kinachostahili au kujiendeleza
kufikia ngazi ya juu zaidi ya stashahada.
“Asilimia 90 ya watangazaji wasio na
taaluma ni sehemu ya wanahabari walio katika vyombo vya habari vya
kielektroniki, lakini wapo katika magazeti pia, hivyo si vyema kuiacha
fursa hiyo ipotee kwa anayependa kuendelea kubaki katika taaluma ya
habari baada ya muda huo kupita.
Kwa mujibu wa Dk Abbas, taaluma ya
habari itaheshimika, weledi kukuzwa na maadili kuzingatiwa, ikiwa
wanahabari watafikia viwango vya elimu vinavyokubalika katika tasnia
hiyo, tofauti na ilivyo sasa ambapo baadhi ya watu wanafanya kazi ya
kutangaza na kuandika habari bila kuwa na elimu yoyote ya Habari.
Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji la
Taifa (TBC1), Ayoub Rioba, alilieleza HabariLeo kuwa wasio na viwango
vya elimu ya Habari vinavyotakiwa hawapaswi kuogopa kwenda kusoma, kwa
sababu Uandishi wa Habari na Utangazaji ni taaluma inayompasa mtu kuwa
na viwango vya elimu vinavyokubalika kisheria.
Alisema tofauti na ilivyokuwa zamani,
utangazaji kwa sasa unachukuliwa kama ubunifu pekee unaotumika kuvuta
watu, bila kuangalia misingi ya uandishi wa habari na maadili,
yanayowalinda watangazaji na wananchi wanaofikishiwa habari hizo pia.
Dk Rioba alisema, “ubunifu pekee
hautoshi, misingi ya Uandishi wa Habari na maadili vinahitajika pia,
hivyo watu wasitafute mashauriano yasiyowasaidia katika hilo au kupiga
kelele, bali waende kusoma na kuhakikisha wanapata elimu inayotakiwa ili
wawe na weledi pamoja na maadili yanayotakiwa katika taaluma hiyo ya
habari.
Kwa maelezo yake, kukosa elimu ya habari
kunasababisha weledi na maadili kushuka, jambo linalochangia kwa kiasi
kikubwa masafa ambayo ni mali adimu, yatumike vibaya kwa mambo yasiyo ya
msingi, hivyo kupotea bure au kutumika kwa ajili ya kuburudisha tu.
Alisema masafa yanapaswa kutumika
kuelimisha watu masuala mbalimbali ya msingi yakiwemo ya afya, utunzaji
wa mazingira na mengine yenye umuhimu kwa jamii. Naye Katibu Mtendaji wa
Taasisi ya Mfuko wa Tanzania Media Foundation (TMF), Ernest Sungura,
alisema misingi ya taaluma ya habari lazima itambuliwe na nidhamu ya
studio hasa za redio nayo isimamiwe vyema kuepusha matumizi mabaya ya
muda pindi watangazaji wanapokuwa hewani.
Kwa maelezo ya Sungura, hilo
litawezekana endapo wanahabari; waandishi wa kawaida, watangazaji na
wahariri watakuwa na taaluma ya habari huku wakitekeleza wajibu wao kwa
kufuata miongozo itakayowaeleza watangaze nini na wakati gani kwa ajili
ya mamilioni ya watu wanaowasikiliza.
“Muda wa hewani ni mali, hivyo
uheshimiwe. Katika kuzingatia weledi huwa inatakiwa miongozo inayopitia
michakato yote muhimu na kukubalika. Uhariri nao udhibitiwe kuhakikisha
kinachoenda hewani kina faida kwa watu.
Bila elimu ya taaluma ya habari hili
huwa gumu kutekelezwa. Watu waende shule,”alisema. Kadhalika, Mwanazuoni
Robert Mkosamali, ambaye pia ni Mchambuzi wa masuala ya habari nchini,
alisema ni vyema wanaotaka kufanya kazi katika tasnia ya habari
wakatumia muda wa miaka mitano waliopewa kusoma, ili wafanye kazi kwa
weledi, maadili na waweze kujiamini pia.
Mkosamali alisema kuna athari mbaya
kufanya kazi ya uandishi au utangazaji bila kuwa na taaluma hiyo kwa
sababu uwezekano wa kukiuka misingi ya kazi, madili na kupoteza muda
unaopaswa kutumiwa kutangaza mambo ya msingi kwa jamii.
Chanzo-Habarileo