WAKATI
unapozungumzia ‘mama wa mataifa yote’, mtu aliye hai anayeweza kuendana
na wasifu huo, atakuwa Mariam Nabatanzi Babirye mwenye umri wa miaka
37.
Katika umri huo, Mariam amejizolea umaarufu kwa sababu ya idadi kubwa ya watoto aliozaa mwenyewe bila msaada wa mtu.
Si
hivyo tu, idadi hiyo ya watoto 38, unaweza kujiwa na fikira gani kwa
haraka? Aliwazaaje wote hao wakiwa wameuzidi umri wake, jambo ambalo si
la kawaida?
Fikra
za haraka zitakazokujia ni kwamba kila mwaka alizaa mtoto mmoja tangu
akiwa na umri wa mwaka mmoja huku mwingine mmoja akizaliwa mwaka mmoja
kabla ya yeye mwenyewe hajazaliwa.
Inawezekana?
Hapana! Ukweli ni kwamba watoto hao 38 kwa sehemu kubwa amewazaa kama
mapacha, mapacha watatu, wanne na wote walizaliwa nyumbani kwa njia ya
kawaida isipokuwa wa mwisho aliyezaliwa hospitali.
Mwanamke
huyo, aishiye katika Kijiji cha Kambiri, Wilaya Mukono nchini Uganda,
aliozwa bila ridhaa yake tena bila kujua wakati akiwa na umri wa miaka
12 kwa mwanamume mwenye umri wa miaka 40.
Hiyo
ilikuwa mwaka 1993, mwaka uliofuata wakati akiwa na umri wa miaka 14,
alipata seti yake ya kwanza ya watoto wawili mapacha, kisha miaka miwili
baadaye wakafuata mapacha watatu kabla ya mwaka mmoja na miezi saba
baadaye kuongeza seti ya mapacha wanne.
Kwa
ujumla, katika watoto wa Mariam kuna seti sita za mapacha wawili, nne
za mapacha watatu na seti tatu za mapacha wanne na watoto waliozaliwa
mmoja mmoja. Kati ya watoto wake wote wasichana ni 10, wavulana wakiwa
28.
Mkubwa ana umri wa miaka 23 huku mdogo akiwa na umri wa miezi minne.
Mariam
anafichua kuwa alinusurika kifo mwaka 1993 na muda mfupi baadaye
aliozwa kwa mume mwenye wake na watoto wengi, na ambaye ni katili.
“Sikujua
kama nimeozwa. Watu walikuja nyumbani na kuleta vitu kwa baba yangu.
Wakati muda ulipofika ugeni kuondoka, nilidhani nilikuwa namsindikiza
shangazi yangu, kumbe nilipofika mbele alinikabidhi kwa mwanamume huyo.
Wakati
Mariam alipoanza kuzaa seti za watoto, hakuona kama ni ajabu kwa vile
baba yake alikuwa na watoto 45 kutoka wanawake tofauti na wote hao
walizaliwa kama mapacha watano, wanne, watatu na wawili.
Ilipofika
mimba ya sita, Mariam alikuwa tayari na watoto 18 na alitaka kusitisha
kizazi, hivyo alienda hospitali, ambako madaktari walimwambia hawawezi
kumsaidia kwa vile ana kiwango kikubwa cha mayai, ambacho kingemuua
iwapo angeacha kuzaa.
Alijaribu tena kusitisha uzazi alipofikisha watoto 23 lakini alipewa onyo kama hilo kuwa atakufa akijaribu kuacha kuzaa.
“Nilishauriwa
kuendelea kuzaa kwa sababu bila kufanya hivyo ni kumaanisha kifo.
Nilijaribu kutumia kifaa kijulikanacho kama Inter Uterine Device (IUD)
lakini niliugua na kutapika na kukaribia kufa. Nilipoteza fahamu kwa
mwezi mmoja,” anakumbuka.
Ni
baada tu ya kufikisha mtoto wake wa 38, ndipo madaktari walipoweza
kumuondolea kizazi. Na ni uzazi huo pekee ambao alijifungulia hospitali
tangu alipoanza kuzaa miaka 24 iliyopita.
“Nilimuomba
daktari asitishe kizazi ili nisizae zaidi, akaniambia ameshaondoa
kizazi. Hii ilikuwa njia pekee niliyozaa kwa upasuaji kwa sababu
nilikuwa bado dhaifu kutokana na ugonjwa niliougua wakati nilipojaribu
kutumia IUD," anasema.
Mmoja wa watoto wake mapacha wa kwanza ana cheti cha uuguzi na mwingine ujenzi ijapokuwa bado hawajapata kazi.
Watoto wake wengine wako kuanzia chekechea hadi madarasa ya juu ya elimu ya msingi.
Kuhusu
kulisha watoto wake, anasema: “Kila kitu kinatoka mfukoni mwangu
mwenyewe, nanunua kilo 10 za unga wa mahindi kwa siku, kilo nne za
sukari kwa siku na miche mitatu ya sabuni.
“Nahitaji
kuwa na Sh 100, 000 za Uganda (sawa na Sh 62,000 za Tanzania) kwa siku
kutosheleza familia. Mungu amekuwa mwema kwangu, kwa sababu watoto
hawajawahi kulala na njaa."
Mariam
hupata fedha kutokana na kuuza dawa za kienyeji za kutibu maradhi
mbalimbali, shughuli ambayo ameifanya tangu alipokuwa msichana mdogo.
Pia
hufanya vibarua kama vile kusuka nywele, mapambo na kupamba maharusi.
Kwa sasa yuko katika mchakato wa kukusanya fedha kuunganisha bomba la
maji ili afanye biashara kwa vile eneo lao lina uhaba wa maji na dumu
moja la maji huuzwa kwa Sh 800 za Uganda.
“Sidharau kazi yoyote inayoniletea fedha. Ninachojisikitikia ni kuacha shule ila namshukuru Mungu kwa zawadi ya hawa watoto."
Miaka 25 ya ndoa kwa Nabatanzi pia imekumbwa na maumivu na mateso.
“Nimeteswa
mara nyingi na mume wangu; hunipiga wakati ninapojaribu kujadiliana
naye masuala muhimu ya kifamilia, hasa anapokuja nyumbani akiwa amelewa.
“Hatoi
fedha wala mahitaji yoyote ya kifamilia; watoto hawamfahamu vyema kwa
vile hukaa hadi mwaka bila kuja nyumbani na watoto wanapozaliwa huwapa
majina kwa njia ya simu.”
Charles Musisi (23), mwanae mkubwa anasema baba yao ametoweka na wamelelewa kwa mapenzi ya mama pekee.
“Naweza
kukuambia wadogo zangu hawamjui baba jinsi alivyo. Mara ya mwisho
nilimuona wakati nikiwa na umri wa miaka 13 tena muda mfupi usiku na
hatujui furaha ya baba ikoje,”anasema mtoto huyo.
Kwa mujibu wa Nabatanzi mumewe anapokuja nyumbani huvizia usiku mwingi na kutokomea mapema asubuhi.
Kuendelea kwake katika ndoa hiyo kunatokana na ushauri wa shangazi yake kuwa asijaribu kuzaa na wanaume tofauti tofauti.