WALIOONEWA SAKATA LA VYETI FEKI WAKATE RUFAA
Serikali,
imesema watumishi wa umma walioorodheshwa kwenye orodha ya watumishi wa
umma wenye vyeti feki, wakati hawakutakiwa kuwekwa, wakate rufaa.
Kauli
hiyo, ilitolewa jana na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Laurean Ndumbaro, alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari.
“Kama
mtakumbuka, uhakiki wa vyeti feki kwa watumishi wa umma, ulihusisha
vyeti vya kidato cha nne, kidato cha sita, ualimu na taaluma zingine.
“Baada
ya uhakiki huo, iliagizwa watumishi 9,932 waliokuwa na vyeti feki,
waondolewe katika ajira, watumishi 1,538 wenye vyeti vyenye utata kwa
maana kwamba vinatumiwa na watu zaidi ya mmoja, wathibitishe vyeti vyao
kabla ya Mei 15 mwaka huu na mishahara yao isimamishwe hadi uhakiki
utakapokamilika.
“Wale
watumishi 11,596 waliogundulika kuwa na vyeti pungufu, wanatakiwa
kuwasilisha vyeti vyao vikaguliwe kabla ya Mei 15, mwaka huu, vinginevyo
watachukuliwa hatua.
“Lakini,
wale wanaodai kwamba wamewekwa kwenye orodha ya wenye vyeti feki wakati
hawakutakiwa kuwa huko, tunawaomba waandike barua za kukata rufaa kwa
Katibu Mkuu Utumishi kupitia kwa waajiri wao.
“Waajiri
hao, watatakiwa kuwasilisha vyeti hivyo Baraza la Mitihani la Taifa kwa
ajili ya uhakiki zaidi kabla ya Mei 15, mwaka huu.
“Pamoja
na hayo, ieleweke kwamba, baadhi ya watumishi wakati wanaajiriwa,
waliwasilisha vyeti vya matokeo mengine ya sekondari na wakati wa
uhakiki, walionyesha vyeti vingine.
“Lakini, naomba ieleweke kwamba, hakuna mtumishi wa umma mwenye cheti halali atakayeondolewa katika utumishi wa umma.
“Kuhusu suala la mafao ya watumishi hao, hilo tunaliangalia namna ya kulifanya kwa sababu kuna sheria zinazolisimamia,” alisema Dk. Ndumbaro.
Ajira za dharura
Pamoja
na hali hiyo, Dk. Ndumbaro aliwataka wakuu wa idara ambazo huduma zake
zimeathiriwa na zoezi la vyeti feki baada ya watumishi kuacha kazi kwa
kuwataka kuandika barua kwake ili zitangazwe nafasi za ajira za dharura
kwa lengo la kuziba mapengo hayo.
Akizungumzia
wizara ambazo taarifa za uhakiki wake hazikutolewa hivi karibuni,
alisema zitatolewa Mei 10 mwaka huu baada ya uhakiki wake kukamilika.
Katika
hatua nyingine, Dk. Ndumbaro alisema Serikali itaajiri watumishi 1,500
kuanzia sasa hadi mwisho wa Bunge la Bajeti linaloendelea mjini hapa.