Wabunge
wawili waliokuwa mawaziri katika Serikali ya Awamu ya Tano, Nape Nnauye
(Mtama) na Charles Kitwanga (Misungwi) jana waligeuziwa kibao,
wakidaiwa kukiuka maadili ya uongozi baada ya kuzungumza kwa hisia dhidi
ya bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Nape
alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kabla ya kuachwa
katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri, wakati uteuzi wa
Kitwanga ulitenguliwa baada ya kuingia bungeni akiwa amelewa.
Wawili
hao juzi walizungumza kwa hisia kuhusu kiwango kidogo cha fedha
kilichowekwa wakisema hakiwezi kutatua tatizo la maji katika maeneo yao;
Kitwanga akisema yuko tayari kuhamasisha wananchi wake 10,000 kwenda
kufunga bomba la maji linalopita eneo lake.
Nape
, ambaye pia alionekana kuwa na hisia kali, alisema sera ya Tanzania ya
viwanda haitawezekana kama suala la maji halitapewa kipaumbele na
kutengewa fedha za kutosha.
Jana,
mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku, maarufu kwa jina la
Msukuma, alisema wakati akichangia hoja ya bajeti hiyo kuwa kauli za
wawili hao zinaonyesha kuwa kuna haja ya kazi ya uhakiki wa vyeti
kufanyika pia kwa mawaziri.
“Kazi
zilizoahidiwa katika Ilani ni nyingi si moja. Hizi hela ni nyingi
tuunge mkono na wala tusiwasumbue kwa kuzikataa. Tuwape nafasi ili
wakafanye kazi,” alisema Msukuma.
“Lakini
suala langu, nataka kuwazungumzia wana-CCM wenzangu ambao jana
nilisikiliza mchango wa mmoja, Kitwanga analalamika anasema
atawamobilize (atawashawishi) wananchi 10,000 wakazime mashine ya maji
Iherere.
“Nataka
niwaulize nyinyi mawaziri wa Magufuli hivi vile viapo mnavyokula mnajua
maana yake? Kama hamvijui basi sina hakika kama mko sawasawa na kama
hamko sawasawa, (Waziri wa Elimu, Joyce) Ndalichako hebu pitisha
operesheni ya vyeti feki, huenda hapa penyewe kuna feki za kutosha.”
Alihoji sababu za mtu aliyekuwa waziri kusimama bungeni na kusema kuwa alivyokuwa waziri alibanwa kuzungumza.
“Kwahiyo
sisi mambo (ambayo) hatuzungumzi kwa kuwasaidia nyinyi tumebanwa na
nani? Mnasimama mnasema sasa nazungumza na nakwenda kuwahamsisha
wananchi 10,000 wakazime mtambo?” alihoji.
“Hebu
ngoja niwakumbushe tukio la mwaka 2014. Wakati Mheshimiwa Kitwanga
akiwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, alikuja Geita . Mimi kama
mwenyekiti wa CCM wa mkoa nikawaambia wananchi wasitoke mpaka walipwe na
mzungu, yeye akaja akamwambia mkuu wa mkoa hata kama kuna mwenyekiti
wapigwe mabomu na kweli kesho yake tulipigwa mabomu.
“Kwa
hiyo nataka nimwambie Waziri wa Mambo ya Ndani siku akienda kuunganisha
wananchi palepale Misungwi naye apigwe mabomu aonje joto ya jiwe.
Haiwezekani waziri uliyekula kiapo, ukitimuliwa unakuja humu
kutuchanganya, wakati hatujui mambo mliyokuwa mnazungumza kwenye cabinet
(baraza la mawaziri).”
Baadaye alimgeukia Nape.
“Nape
ambaye alikuwa mwenezi wangu wa (CCM) Taifa, jana (juzi) alizungumza
mambo mazuri lakini kuna moja alisema ‘tusipowatekelezea suala la maji
wananchi hawataturudisha tena madarakani’.”
Alisema hilo haliwezekani kwa sababu wananchi wanawategemea kwa mambo mengi na si maji pekee yake na wamewafanyia vizuri.
Alisema ilani hazijaanza kuandikwa katika Serikali ya Awamu ya Tano na suala si kumaliza ahadi zote.
Awali alimpongeza Rais John Magufuli na wizara hiyo kwa kazi aliyoiita kuwa nzuri, akisema ameona mabadiliko makubwa.
“Mimi
niko tofauti kidogo na wabunge wenzangu wanaosema tusipitishe bajeti
kwa sababu hela ni ndogo. Binafsi naona hizi hela ni nyingi sana, tatizo
ni zitoke zote tofauti na bajeti ya mwaka jana.”