Chama
Cha ACT- Wazalendo leo kimemtangaza rasmi Mwanasheria Albert Msando
kuwa mrithi wa nafasi ya Mshauri Mkuu wa Chama hicho iliyoachwa wazi na
Prof Kitila Mkumbo aliyeteuliwa na Rais Magufuli kuwa Katibu Mkuu Wizara
ya Maji.
Akiongea
na waandishi wa habari Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho Dorothy Semu,
amesema Kamati Kuu ya Chama hicho ilikutana tarehe 7 Mei na kufanya
mabadiliko ya kiuongozi ndani ya chama.
"Kama
mnavyofahamu, mnamo tarehe 07 Mei, 2017 Kamati Kuu ya Chama cha ACT
Wazalendo ilikutana katika mkoa wa kichama Kahama na kufanya kikao chake
cha kawaida. Katika kikao hicho, pamoja na mambo mengine yaliyojadiliwa
na kufikiwa maamuzi, Kamati Kuu ilifanya mabadiliko kadhaa ya safu ya
Uongozi wa juu Makao Makuu ikiwemo kuthibitisha uteuzi wa Mshauri wa
Chama wa masuala ya kisheria. Lengo kuu la mabadiliko yaliyofanywa na
Kamati Kuu ni kuleta ufanisi wa utekelezaji wa kazi na majukumu ya
Kamati za kisekta Makao Makuu ya Chama na mikoani" alisema Dorothy Semu
Mbali na hilo Dorothy Semu anasema kwa kauli moja Kamati kuu ilikubaliana na mapendekezo ya kiongozi wa chama.
"Kwa
dhamana aliyonayo kikatiba kwa mujibu wa ibara ya 29(25)(vii), Kiongozi
wa Chama aliona umuhimu wa Chama kuwa na Mshauri wa Masuala ya Sheria
na akapendekeza jina la ndugu Albert Msando kuwa Mshauri wa Chama juu ya
mambo ya Sheria na kuliwasilisha mbele ya Kamati Kuu. Kamati Kuu kwa
kauli moja ilikubaliana na mapendekezo hayo na ikapitisha uteuzi huo kwa
mujibu wa Katiba ibara ya 29(13)(ii). Uteuzi wa Ndugu Msando umeanza
rasmi tarehe 08 Mei 2017" alisisitiza Dorothy Semu