MAFURIKO YA VYETI FEKI YAHAMIA BARAZA LA MITIHANI TANZANIA - NECTA
BARAZA la Mitihani Tanzania (NECTA) limeendelea kupokea umati wa
watumishi wa umma waliojitokeza kukata rufaa na kuhakiki vyeti vyao
ambao majina yao yalibainishwa kwenye orodha iliyotolewa na serikali ya
watumishi walioghushi vyeti.
Gazeti la Habarileo lilishuhudia umati huo wa watumishi ukiwa
umekusanyika katika ofisi hizo za Necta zilizopo Mikocheni jijini Dar es
Salaam huku baadhi yao waliowahi wakipewa namba na kuingia ndani
kuwasilisha vyeti na wengine wakisubiri nje kupangiwa utaratibu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Ofisa Habari wa baraza hilo, John
Nchimbi alikiri baraza hilo kupokea umati mkubwa wa watumishi hao
wanaokata rufaa ambao wanaongezeka kila siku.
Nchimbi alisema kwa sasa kuna makundi matatu ya watumishi hao yakiwemo
kundi la watumishi walioghushi vyeti, watumishi waliowasilisha vyeti
visivyokamilika na watumishi wenye vyeti vyenye utata ambavyo cheti
kimoja kinatumiwa na zaidi ya mtumishi mmoja.
“Kiutaratibu sisi Necta tunatakiwa kuwashughulikia watumishi waliopo
kwenye orodha ya vyeti vyenye utata, tunamtaka mtumishi aliyekata rufaa
awasilishe vyeti vyake halali kwetu tunampa namba na anaondoka zake,”
alisema Nchimbi.
Hata hivyo, alifafanua kuwa pamoja na ukweli huo, makundi yote matatu
yamejitokeza na kuwasilisha rufaa na malalamiko yao Necta jambo ambalo
baraza hilo inabidi liwahudumie.
Alisema kiutaratibu watumishi ambao vyeti vyao havijakamilika,
wanatakiwa kuwasilisha rufaa zao kwa waajiri wao na vielelezo baada ya
hapo waajiri hao watawasilisha mbele ya baraza hilo rufaa hiyo
iliyoambatana na vielelezo.
Kwa upande wa watumishi wenye vyeti vya kughushi wanapaswa kuwasilisha
rufaa zao kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala wa Bora ambaye ndiye atakayewasilisha rufaa hizo kwa
baraza hilo la mitihani.
“Bahati mbaya kwa sasa wote wanakuja kwetu lakini tunawahudumia,
tunajitahidi kuhakikisha kila mtu anapata haki yake, utaratibu mzijma
ukikamilika kwa tarehe iliyotangazwa na Rais John Magufuli, tutapeleka
idadi ya waliokata rufaa na matokeo kunakohusika,” alifafanua.
Baadhi ya watumishi waliojitokeza katika eneo hilo la Necta, walioomba
kutotaja majina yao kwa usalama wao kikazi, walibainisha kuwa wameamua
kukata rufaa kwa kuwa wana uhakika hawajaghushi vyeti vyao.
“Mimi nimeshangaa kuliona jina langu kwenye orodha ya walioghushi kwanza
nimeshtuka sana, nimeambiwa vyeti vyangu vinatumiwa na watu wengine
ambao hata siwajui, nimekuja hapa kuthibitisha kuwa mimi ndio mmiliki
halali wa vyeti vyangu,” alisema mmoja wa watumishi hao aliyetambulisha
kuwa anafanya kazi kwenye halmashauri.
Kwa upande wake, mtumishi mwingine aliyedai kuwa ni mwalimu, alipongeza
utaratibu uliowekwa na Necta wa kusikiliza malalamiko ya watumishi na
kubainisha kuwa tangu afike hapo baada ya kupewa namba amefanikiwa
kuwasilisha vyeti vyake na sasa anasubiri matokeo.
Hata hivyo, mtumishi huyo alionyesha wasiwasi juu ya ajira yake na
kubainisha kuwa kuwa kwa kuwa jina lake limeshaondolewa kwenye mfumo wa
malipo wa mwajiri wake, huenda ikachukua muda mrefu kurejeshwa tena
hivyo hali yake kimaisha kuzidi kuwa ngumu.
Kwa upande wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), gazeti hili
lilimtafuta Mkurugenzi Mtendaji, Profesa Lawrence Museru pamoja na Ofisa
Habari wa hospitali hiyo, Aminiel Eligaesh kwa ajili ya kupata
ufafanuzi juu ya athari zilizopatikana baada ya watumishi wa hospitali
hiyo 134, kusimamishwa kazi kwa kughushi vyeti, bila mafanikio jana kwa
kuwa viongozi hao walikuwa kwenye kikao kutwa nzima.
Juzi hospitali hiyo ilitoa orodha na vitengo vya watumishi wake 134
waliobainika kughushi vyeti vya sekondari na kutangaza wazi kuwa
wamekosa sifa ya kuwa watumishi wa umma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Angela
Kairuki hivi karibuni alitoa orodha ya watumishi 9,932 wanaodaiwa
kughushi vyeti ambao kwa mujibu wa Dk Magufuli aliwapa muda wa siku 14,
kujiondoa kazini na wale wataokaidi watachukuliwa hatua za kisheria
ikiwemo kifungo cha miaka saba jela.
Hata hivyo, ikiwa imepita wiki moja tangu kutolewakwa orodha hiyo, juzi
Katibu Mkuu wa Utumishi, Dk Lauren Ndumbaro alitoa tena orodha ya
watumishi 2,016 wanaodaiwa kuwasilisha vyeti visivyokamilika.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, watumishi hao ambao wengi wao wanatokea
kwenye taasisi na mashirika ya serikali, wametakiwa kuhakikisha hadi
mwishoni mwa mwezi huu, wawe wamewasilisha vyeti vyote vilivyokamilika
ndipo watakapothibitishwa utumishi wao.
Katika hatua nyingine, Mwandishi Wetu Lucy Ngowi anaripoti kuwa
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, imeondokewa na
watumishi 383 ambao wamebainika kuwa na vyeti vya kughushi pamoja na
vile vyenye utata baada ya kufanyika kwa uhakiki wa vyeti kwa watumishi
wa umma.
Watumishi walioondoka wametokea idara za elimu, uhasibu, biashara,
uvuvi, afya, sheria, maendeleo ya jamii na utawala. Kuondoka kwa
watumishi hao kumeilazimu manispaa hiyo kubadili utaratibu wake kwa
kuwarudisha kazini wote waliokuwa likizo pamoja na kuondoa shifti tatu
na kubakiza shifti mbili inayowalazimu wafanyakazi kufanya kazi kwa saa
12.
Kwenye elimu manispaa hiyo imehamisha walimu kujaza nafasi katika shule
zilizokuwa na uhitaji zaidi, na kwenye malindo wameongeza nguvu kwa
kutafuta vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Msongela Palala alisema jana
alipozungumza na gazeti hili kuhusu wafanyakazi hao waliogundulika
katika manispaa yake. Alikiri kuwa kuondokewa kwa watumishi hao
kumeiathiri manispaa hiyo kwa kuwa walimu wa msingi pekee waliokumbwa na
sakata hilo idadi yao ni 165, madaktari watatu kutoka Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa Amana na mmoja katika Hospitali ya Mnazi Mmoja.
Vilevile madaktari wasaidizi sita, matabibu, maofisa uuguzi hivyo
kufikisha sekta hiyo ya afya kufikia 98. Alisema watumishi kutoka
utawala, maendeleo ya jamii, sheria, ujenzi, mipango miji na ugavi
wamefikia 38.
Mkurugenzi huyo alisema watumishi waliogundulika vyeti vya kugushi
katika awamu ya kwanza walikuwa 330, awamu ya pili wale wenye vyetu
vyenye utata ni 53. Alisema miongoni mwa watumishi hao waliokumbwa na
sakata hilo wengi wao hawana vyeti vya kidato cha nne kwa kuwa ajira zao
hazikuwataka wapeleke vyeti hivyo kwa mfano walimu wa UPE pamoja na
wauguzi wa afya ambao hawakuwa ni lazima wawe na cheti hicho cha kidato
cha nne.
Alisema kutokana hali hiyo manispaa hiyo imejipanga kuboresha kwenye
maeneo yaliyoathirika kama elimu pamoja na afya. “Kwenye elimu
tumejipanga vizuri katika maeneo yaliyoathirika zaidi kwa kuwahamisha
walimu kutoka sehemu ambazo hazina uhitaji na kuwapeleka kwenye mahitaji
zaidi,” alisema na kuongeza shule ya sekondari ya Pugu wamepeleka ofisa
ugavi kwenda kusaidia baada ya aliyekuwepo naye kukumbwa katika sakata
hilo.
IMEANDIKWA NA HALIMA MLACHA- HABARILEO