ALIYEKUWA Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, ametishiwa kufyatuliwa risasi na askari polisi.
Hili
ni tukio la pili kutokea baada ya aliyekuwa Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, kutishiwa bastola hadharani.
Katika
video iliyoanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii jana, linaonekana
gari aina ya Land Cruiser lenye namba T 296 ATW, ambalo liliegeshwa
pembeni kisha wakashuka askari wawili – mmoja wa Kikosi cha Kutuliza
Ghasia (FFU) na mwingine polisi wa kawaida.
Askari
huyo wa FFU baada ya kushuka kwenye gari hilo, alinyanyua bunduki na
kufyatua risasi hewani kabla mwenzake kumfwata na kumshika kifuani na
kutaka kumrudisha katika gari.
Kisha
alimfuata Malima na kuzungumza naye na wakati wakiendelea, yule askari
aliyefyatua risasi naye alikuja na kumsukuma mara mbili waziri huyo wa
zamani, kisha akanyanyua bunduki juu.
Askari
huyo alisikika akitamka: “Kwanini hamuheshimu, kwanini hamuheshimu
Serikali nyie, mzee heshimu Serikali, mimi nimewekwa kuitumikia
Serikali, siwezi kudharaulika.”
Mtu mwingine wa pembeni ambaye hakuonekana katika video hiyo, alisikika akisema: “Huna mamlaka, huna mamlaka ya kutishia.”
Wakati wote huo, Malima alionekana akiwa ameweka mikono mfukoni mwa suruali yake.
Baada ya majibizano, mmoja wa askari alionekana akimsihi mwenzake waende katika gari, huku akitamka “Poti, Poti, Poti ee.”
CHANZO CHA TUKIO
Taarifa
za ndani zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea katika eneo la Masaki
jijini Dar es Salaam jirani na Hoteli ya Double Tree, ambako dereva wa
Malima aliegesha gari vibaya.
Hatua
hiyo ilisababisha kutokea kwa majibizano kati ya maofisa wa Kampuni ya
Udalali ya Majembe kabla polisi kuingilia kati na kufyatua risasi juu.
Inaelezwa kuwa Malima alifika akiwa kwenye gari jingine na kukuta mzozo unaendelea.
KAULI YA POLISI
Akizungumza na MTANZANIA, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Suzan Kaganda, alisema ufafanuzi kuhusu tukio hilo utatolewa leo.
Pia alisema wanaendelea kumhoji Malima katika Kituo cha Polisi Oysterbay.
“Polisi
walikuwa wanafanya ukamataji, lakini tukio litatolewa ufafanuzi kesho
(leo)… kuna mambo mawili, kuna kumshikilia na kumhoji, sisi tunamuhoji,”
alisema Kaganda.
WAZIRI MWIGULU
MTANZANIA
lilipomtafuta kwa simu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu
Nchemba kuzungumzia tukio hilo, aliomba atumiwe ujumbe mfupi na hata
alipotumiwa hakujibu.
LEMA AONYA
Akizungumza
na MTANZANIA, Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema,
alisema roho za visasi zinaendelea kujengwa kati ya raia na polisi na
hivyo taifa linakoelekea ni kubaya kwani litapoteza dira na amani.
“Nimesikitika
na nampa pole Malima, matukio ya aina hii yako mengi. Kama imefika
mahali tunatoleana SMG hadharani, hakuna mtu ambaye yuko salama katika
nchi hii,” alisema.
Lema
alikwenda mbali na kugusia matukio yaliyowahi kutokea, likiwamo lile la
aliyekuwa Waziri wa Habari, Nape na kusema kuwa hata aliyemtishia
bastola hajakamatwa.
“Kama
kusipokuwa na udhibiti watu watauana hadharani, tukio la kubishania
parking (maegesho) si la kurushiana risasi, ni suala la maelewano tu,”
alisema.
TUKIO LA NAPE
Machi
23, mwaka huu, Nape alitishiwa bastola akiwa nje ya Hoteli ya Protea
jijini Dar es Salaam, alipotaka kuzungumza na waandishi wa habari.
Tukio hilo lilitokea saa chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kumvua uwaziri.
Nape
alipanga kuzungumza na vyombo vya habari, lakini harakati zake zilitiwa
dosari, ikiwamo kuzuiwa kufanya mkutano ndani ya Hoteli ya Protea na
kuamua kuzungumza nje ya hoteli hiyo.
Hata
hivyo, kabla ya kushuka katika gari kuzungumza na vyombo vya habari,
alifuatwa na watu wawili waliodaiwa kuwa ni askari na kutaka kumzuia
asishuke.
Mmoja wa watu hao alichomoa bastola na kumtishia.
Na NORA DAMIAN-MTANZANIA DAR ES SALAAM