Zacharia Hans Poppe, mmoja wa wanachama na viongozi maarufu wa Klabu ya Simba, ameamua kuachia ngazi kwenye kamati ya utendaji.
Uamuzi wake wa kuondoka kamati ya utendaji, moja kwa moja unamuondoa kwenye nafasi ya mwenyekiti wa kamati ya usajili.
Hans
Poppe amesema kuwa, ameondoka baada ya jopo lililoongozwa na Rais wa
Simba, Evans Aveva kuingia mkataba na Kampuni ya Michezo ya Kubashiri ya
SportsPesa ambao wamesaini mkataba wa Sh bilioni 4.9 kwa miaka mitano.
Akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti hili, Hans Poppe amesisitiza, ameamua kukaa pembeni.
“Nitabaki
kama mwanachama wa kawaida wa Simba. Nitaendelea na shughuli zangu
nyingine,” alisema na alipoulizwa sababu za kujiuzulu alisema.
“Mambo
yamekwenda kwa uficho, mkataba umekuwa ukifichwa. Kamati ya utendaji
imetaarifiwa siku moja kabla ya kusainiwa. Ilikuwa Alhamisi, Ijumaa
wamesaini, nini kinafichwa.
“Mimi
nakaa pembeni, nimeshaandika na barua. Sitaki kuwa sehemu ya watu wasio
waungwana. Angalia hata Mo Dewji hakuwa akijua, lakini huyu mtu mwaka
mzima ndiye katukopesha mishahara.
“Dewji
alisema, mkitaka kusaini mkataba kama mmepata mdhamini mniambie. Maana
na yeye tulimpa jukumu la kutafuta mdhamini, hata mimi nilipewa jukumu
hilo lakini leo unasikia wenzako wameingia mkataba na mdhamini mpya.
“Kabla tumekuwa tukishirikiana kwa kila jambo, kwenye shida na raha. Vipi leo, nini kimefanya tusiwe pamoja?
“Kawaida
walitakiwa waje na mkataba, tuujadili na kuangalia vipengele. Kama kuna
sehemu zikarekebishwe au kuongezwa vifanyiwe kazi, mwisho wakija tuseme
hapa sawa, basi usainiwe. Nani atakataa mdhamini kama unaona ana faida
na klabu?” alihoji Hans Poppe.
Hans Poppe ndiye amekuwa injini ya usajili katika usajili katika kikosi cha Simba.