BUNGE LA TANZANIA LAKATAA MAJINA YA WAGOMBEA WA CHADEMA NA CUF KUGOMBEA UBUNGE AFRIKA MASHARIKI
Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limekataa majina ya wagombea wa
CHADEMA na CUF kwenda kugombea nafasi ya Ubunge wa Afrika Mashariki
(EALA) baada ya kukutwa na mapungufu katika fomu zao.
Hatua
hiyo imekuja baada ya wagombea hao kuonekana na mapungufu mbalimbali
yaliyobainika kwenye nyaraka zao a uteuzi yakiwa yamekiuka masharti ya
Ibara ya 50 ya Mkataba wa Kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki,
Ibara ya 67 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Kifungu cha
4(4) cha Sheria ya Uchaguzi wa wajumbe wa Bunge la Afrika Mashariki ya
Mwaka 2011 iliyotungwa na Bunge la Afrika Mashariki.
Aidha
taarifa hiyo imesema CHADEMA uteuzi wao haukuzingatia jinsia, lakini
pia hawajaambatanisha fomu za maombi ya wagombea, orodha ya waombaji
pamoja na fomu ya matokeo ya kura.
Huku
CUF wakiwa wametuma fomu za uteuzi wa wagombea zikiwa zimewasilishwa na
mamlaka mbili tofauti, wagombea wawili hawana uthibitisho wa uraia wao,
fomu za uthibitisho wa hiari ya kugombea haikuwepo kwa wagombea wote,
orodha ya waombaji haipo kwa mgombea mmoja, fomu ya matokeo ya kura kwa
wagombea haikuwepo pamoja na fomu ya mahudhurio kwa mgombea mmoja
kutotimia.
Kutokana
na mapungufu hayo msimamizi wa Uchaguzi Dr. Thomas D. Kashililah
amesema ameshindwa kufanya uteuzi huo huku akiwataka kurekebisha
mapungufu yaliyobainishwa kabla ya saa 7 mchana, Aprili 4 ofisini kwake
mjini Dodoma.
Kwa
upande mwingine amewashukuru wadau wote hususani vyama vyote vya siasa
nchini kwa ushirikiano mzuri waliyompa katika zoezi zima la mchakato wa
uteuzi wagombea pamoja na vyombo vya habari kwa ujumla.