Waziri Nape Awataka Maafisa Mawasiliano Serikalini Kutendea Haki Sheria Ya Huduma Za Habari Na Sheria Ya Haki Ya Kupata Taarifa.
![]() |
Mkurugenzi wa Idara
ya Habari-MAELEZO Dkt Hassan Abbas akichangia jambo wakati wa kikao cha 12 cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali kinachofanyika Mkoani Dodoma.
|
![]() |
: Mkuu wa Wilaya ya
Bahi Bi.Elizabeth Kitundu akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kikao kazi cha 12
cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali kinachofanyika Mkoani Dodoma.
|
![]() |
Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO)
akichangia jambo wakati wa Kikao kazi cha 12 cha Maafisa Mawasiliano wa
Serikali kinachofanyika Mkoani Dodoma.
|
Habari na:
Lorietha Laurence – Dodoma.
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye amewataka Maafisa
Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini kuzisoma, kuzielewa na kuzifanyia
kazi sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na ile ya Haki ya kupata Taarifa ya mwaka 2016 ili kuweza kutekeleza majukumu
yao kwa ufanisi katika kuuhabarisha umma.
Waziri
Nape ameyasema hayo leo Mjini Dodoma alipokuwa akifungua mkutano wa Maafisa
Mawasiliano Serikalini ambapo licha ya kuwataka kuzijua sheria hizo pia
amewataka kuwa wabunifu kuendana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika
utendaji kazi wa kila siku.
Aidha
aliongeza kuwa kuwepo kwa sheria hizo mbili kutatengeneza daraja
litakalounganisha na kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa wananchi.
“Ni
wajibu wa Maafisa Mawasiliano kuzijua na kuzitendea kazi sheria hizi ili
kurahisisha upatikanaji wa mawasiliano baina ya serikalini na umma hivyo
kuondoa ugumu uliokuwepo hususani katika kupatikana kwa taarifa muhimu kwa
wananchi”
alisema Waziri Nape.
Aliongeza
kwa kufafanua kuwa endapo utekelezaji wa sheria hizi mbili muhimu utasimamiwa
na kuzingatiwa basi kutakuwepo na matokeo chanya ya kiutendaji na hivyo kuleta
mafanikio makubwa yanayotarajiwa na umma.
Waziri
Nape pia aliwataka Maafisa Mawasiliano hao kuwa wabunifu katika utekelezaji wa
majukumu yao kwa kuendana na maendeleo ya teknolojia ikiwemo matumizi ya
mitandao ya kijamii katika kuhabarisha umma na kutoa taarifa kwa wakati.
“Zama
hizi sio zile za maafisa mawasiliano kujisifia kwa kuwa na safari nyingi badala
yake kuwa watekelezaji wa kazi zao kwa wakati na matokeo yanayoonekana kwa umma
ila kwa atakayeshindwa kutekeleza hayo basi tutaomba atupishe”
alisema
Waziri Nape.
Aidha
alieleza kuwa anafahamu kuwa kuna changamoto nyingi ambazo maafisa mawasiliano
wanakumbana nazo katika utendaji wao wa kazi ikiwemo ukosefu wa vifaa ingawa si
kigezo cha wao kutokutekeleza wajibu wao.
Katika
kuhakikisha kuwa changamoto ya ukosefu wa vifaa inatatuliwa Waziri Nape alitoa
Wito kwa Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuweka
kipaumbele katika bajeti hii mpya kwa kutenga kiasi cha fedha ambacho kitasaidia
kununua vifaa kwa ajili ya Maafisa Mawasiliano wa Wizara, Taasisi, Mikoa,
Wilaya na Halmashauri .
Naye
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bibi. Nuru Millao
alisema kuwa umuhimu wa mkutano wa Maafisa Mawasiliano Serikalini ni katika
kuwajengea uwezo wa kiutendaji pamoja na kutathmini utendaji kazi wao.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Elizabeth Simon Kitundu
ameishukuru Wizara kuandaa mafunzo kwa Maafisa Mawasiliano Serikalini na
kuyafanyia Mkoani Dodoma kwani kwa kufanya hivyo itarahishisha mfumo wa
kimawasiliano na kutangaza fursa zilizopo Mkoani Dodoma hivyo kuwafanya
watumishi wa umma kuwa na amani katika kutekeleza agizo la kuhamia Dodoma.
Mkutano
wa Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini umefanyika kwa mara ya 12
huku lengo ikiwa ni kuwakutanisha kwa pamoja maafisa hao kutoka katika ngazi
mbalimbali za kiutendaji serikalini ikiwemo Wizara, Idara, Taasisi, Mikoa,
Wilaya na Halmashauri ili kuweza kubadilishana uzoefu wa kiutendaji pamoja na
kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.






