LAPF YAKUSANYA ZAIDI YA BILIONI 281
|
Meneja Mafao
wa Mfuko wa Pensheni wa LAPF Bw. Ramadhani Mkeyenge akiwaeleza waandishi wa habari
leo Jijini Dar es salaam (hawapo
pichani) kuhusu utendaji wa mfuko huo
kwa kipindi cha mwaka 2015/2016. Kushoto ni
Afisa Masoko Mwandamizi Bi.
Rehema Mkamba.
|
Afisa
Matekelezo Mwandamizi kutoka Mfuko wa
Pensheni wa LAPF Bw. Kafiti Kafiti (kulia)
akieleza kwa waandishi wa habari kuhusu fursa wanazopata wanachama waliojiunga
na mfuko huo. Alioambatana nao pichani ni Maafisa Waandamizi wa mfuko huo.
(Picha na
Fatma Salum)
Na Frank
Mvungi
Mfuko wa
Pensheni wa LAPF umekusanya shilingi zaidi ya bilioni 281 katika kipindi cha
mwaka 2015/2016 ikiwa ni sehemu ya mikakati ya mfuko huo kupanua huduma zake na
kuwafikia watanzania wengi hasa wanaoishi pembezoni.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam Meneja Mafao wa Mfuko huo Bw.
Ramadhani Mkeyenge alisema ni dhamira ya mfuko huo kuwainua wananchi kwa
kuwasogezea huduma karibu na maeneo yao.
“Dhamira
yetu ni kuhakikisha tunawawezesha wananchi kiuchumi kwa kufanya kazi kwa
uadilifu, ufanisi, ari na ujuzi na tumekuwa tukifanya hivi kwa zaidi ya miaka
70” Alisisitiza Mkeyenge.
Akifafanua
Mkeyenge alisema kuwa mafao yanayotolewa na mfuko huo ni pamoja na pensheni ya
uzee, pensheni ya warithi, pensheni ya ulemavu, mafao ya uzazi, msaada wa
mazishi na mafao ya kujitoa.
Akizungumzia
mikakati mingine ya kuwawezesha wananchi, Mkeyenge alisema mfuko huo unatoa
mikopo ya elimu, mikopo ya saccos, mikopo ya nyumba na mikopo ya wastaafu.
Katika
kusogeza huduma zake karibu na wananchi LAPF imekuwa ikiandikisha wanachama
kutoka sekta zote binafsi na Serikalini na inajivunia kuwa na ongezeko la
wanachama.
Ongezeko hilo
linatokana na fursa waliyonayo wanachama ya kuchagua mfuko wanaotaka na ubora
wa huduma na mafao yanayotolewa na LAPF.
Hatua
nyingine ni kutanua wigo wa wachangiaji kwa kuwafikia wale ambao wako kwenye
ajira binafsi kupitia Mpango wa Akiba ya Hiari wa LAPF.
LAPF ina
wanachama zaidi ya 165,000 nchi nzima na imefanikiwa kufungua ofisi mpya kanda
ya magharibi katika Mkoa wa Geita ili kusogeza huduma katika mikoa ya Geita,
Kagera na Kigoma.