Waziri Mkuu awapa onyo wakadiriaji majengo nchini
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi
wajiepushe na vitendo vya rushwa ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa
inalingana na thamani ya fedha inayotumika.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo jana wakati akifungua semina endelevu ya 29 ya
Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi, iliyofanyika
Jijini Dodoma.
’’Epukeni
vitendo vya rushwa ambavyo huisababishia Serikali hasara kubwa na
kuleta usumbufu kwa wananchi. Ni matumaini yangu kuwa mtafanya kazi kwa
weledi na kufuata maadili ya taaluma zenu’’ Majaliwa.
Alisema
wataalamu hao ni vema wakahakikisha majengo wanayobuni yanakuwa bora
katika muonekano na mandhari yake iwe yenye kuvutia na yenye kuzingatia
utunzaji wa mazingira na matumizi bora na endelevu ya nishati.
Aidha
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Bodi ya Usajili wa Wabunifu
Majengo na Wakadiriaji Majenzi kwa kuchagua mada inayohusu jukumu la
wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi katika kuendeleza viwanda hapa
nchini.
Alisema
anatambua kuwa ujenzi wa viwanda unaendana na ujenzi wa miundombinu
kama majengo, barabara, madaraja, miundombinu ya nishati na viwanja vya
ndege, ambayo ni muhimu katika kuimarisha uchumi wa viwanda.
"Hivyo,
wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi mna mchango mkubwa sana katika
kufikia uchumi wa viwanda. Nitoe rai kwa Bodi ihakikishe kuwa miradi
yote ya majengo pamoja na miundombinu mingine inashirikisha wabunifu
majengo na wakadiriaji majenzi katika ubunifu na usimamizi wa ujenzi
wake.’’