Wanaume Waliokaidi Wito wa Makonda Waanza Kusakwa
Jeshi
la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limeanza kuwasaka wanaume
zaidi ya 1,000 waliokaidi wito wa kufika kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam Paul Makonda, baada ya kudaiwa kutelekeza watoto.
Wanaume
hao ni miongoni mwa waliotajwa na wanawake waliofika kwa Makonda kuomba
msaada wa kisheria baada ya kudai kutelekezwa na wenzi wao.
Jumla
ya wanawake 17,000 walifika katika ofisi hizo kwa ajili ya kuomba
msaada wa kisheria, lakini kutokana na wingi huo ni 7,000 waliohudumiwa.
Makonda
aliwaita wanawake na wanaume wenye watoto ambao walitelekezwa na wenza
waliozaa nao kwa siku 15 katika ofisi zake jijini Dar es Salaam na
wanaume 2008 waliridhia kulea watoto wao.
Mkuu
wa Mkoa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akitangaza
kamati aliyoiunda kuchunguza tatizo la watoto kutelekezwa, iliyohusisha
wanasheria, maofisa ustawi wa jamii na wadau wengine, inayoongozwa na
Mwanasheria na Wakili wa Kujitegemea, Albert Msando.
Kamati
hiyo yenye wajumbe 11 imepewa mwezi mmoja na itawahoji wananchi
waliofika katika ofisi hizo kupata msaada wa kisheria ili kujua
wanavyohudumia kwenye ngazi ya Ustawi wa Jamii kabla ya kufika hapo,
namna kesi za watoto zinavyoendeshwa na kama sheria iliyopo ina
upungufu.
Makonda
alisema kati ya idadi ya wanaume hao wapo waliokamatwa kutoka ndani na
nje ya mkoa wa Dar es Salaam na kwamba kazi hiyo inaendelea.
“Zoezi
la kuwakamata wanaume ambao walikaidi agizo la kuitikia wito wangu
linaendelea na tayari nimeshakabidhi majina zaidi ya 1,000 kwa Kamanda
wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa na wengine
wameshaanza kukamatwa na wapo kutoka mikoa mbalimbali,” alisema Makonda.
Alisema wapo wanaume waliojitokeza kuitikia wito katika siku ambazo walishafunga kutoa huduma ili nao wasikilizwe.
Aidha
alisema katika usikilizaji huo jumla ya familia 4,644 ziliruhusiwa
kumaliza kesi zao katika ngazi za manispaaa huku watu 10,000 wakikosa
huduma kutokana na ofisi yake kuelemewa na idadi ya watu.
“Sikuweza
kuhudumia watu wote waliojitokeza kwasababu walikuwa wengi kuliko uwezo
wangu, hivyo watu 10,000 hawakupata huduma na ndiyo sababu ya kuunda
kamati hii ili kupata ufumbuzi wa kudumu,” alisema Makonda.
Pia
alisema alizisaidia kupata mawakili ambao hawatawatoza fedha familia
zaidi ya 100 ambazo ziliamua kumaliza matatizo hayo mahakamani.
“Wanawake
wanapata shida na watoto hata wakitaka kudai haki zao mahakamani
hawawezi kupata kwa sababu mawakili wanataka fedha kwa hiyo wanawake 100
waliamua kwenda mahakamani nimewatafutia mawakili wa kuwatetea bure,”
alisema Makonda.
Aidha,
alisema kutokana na kuwapo kwa wimbi la wazazi kutelekeza watoto, kuna
ongezeko la zaidi ya watoto 5,000 wa mitaani katika Jiji la Dar es
Salaam.
Alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo ndiyo sababu amekuwa akitafuta mbinu mbalimbali za kulitatua na si kupunguza tatizo.
“Watu
wanasema Makonda anaanzisha mambo na kuyaacha bila kumalizika, mimi
nawaeleza kuwa si kweli, suala hili nilianza nalo kwa kuwaondoa watoto
wanaoomba omba barabarani na hii ni sehemu ya nne ya mwendelezo wake,”
alisema Makonda.
Pia
Makonda alisema baada ya kamati hiyo kukamilisha kazi yake,
wataiwasilisha ripoti hiyo kwa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi), Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na
Watoto na Wizara ya Katiba na Sheria ili mapendekezo yake yaweze
kufanyiwa kazi.
Naye
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Wakili Msando, aliahidi kuwa ataifanya kazi
hiyo kwa uaminifu na uadilifu mkubwa kuanzia jana ingawa ni kazi ngumu.