Waziri Mkuu Ashiriki Ujenzi Wa Uwanja Mpya
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ameshiriki kazi za ujenzi wa uwanja mpya wa
michezo wilayani Ruangwa kwa kubeba zege na matofali pamoja na wananchi.
Waziri
Mkuu ambaye pia ni mbunge wa Ruangwa, ameshiriki zoezi hilo jana
(Ijumaa, Mei 25, 2018) kwenye uwanja huo unaojengwa katika kijiji cha
Dodoma, kata ya Nachingwea, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Akizungumza
na wananchi na viongozi waliojitokeza kushiriki zoezi hilo, Waziri Mkuu
amesema ameridhishwa na kazi ya ujenzi inayoendelea hadi sasa na
akatumia fursa hiyo kuwashukuru wana-Ruangwa kwa kurejesha moyo wa
kufanya kazi kwa kujitolea.
“Ninawashukuru
sana wana-Ruangwa kwa sababu mmeanza kufanya kazi za kujitolea, haya
matofali ni matokeo ya kazi yenu, hakuna hata mtu mmoja amelipwa kwa
kazi hii. Nimeambiwa yanahitajika matofali 60,000 kwa ajili ya kujenga
uzio lakini hadi sasa mmeshafyatua 57,000 na zaidi, ninawashukuru sana,”
amesema.
“Nimeambiwa
madiwani walipiga kambi ya wiki moja hapa, Umoja wa Vijana wa CCM nao
walipiga kambi, UWT walikuja kusomba matofali, watumishi wa Halmashauri
nao walipiga kambi, hongereni sana kwa kurejesha moyo wa kujitolea
miongoni mwa wananchi,” amesema.
Katika
zoezi la leo, walijitokeza wananchi wengi wakiwemo wazee, vijana na
watoto. Baadhi ya watoto walikuwa wakibeba tofali moja kwa kushirikiana
wawili wawili, watatu watatu hadi wanne.
Alisema
ujenzi wa uwanja huo hadi sasa umeungwa mkono na wadau mbalimbali
ambapo aliishukuru Benki ya CRDB ambayo imetoa sh. milioni 15
zilizotumika kununua mifuko ya saruji 1,200; Mbunge wa Kwimba, Bw.
Mansoor Shanif Hiran mifuko 1,200 ya saruji; Mtibwa Sugar mifuko 2,000
ya saruji na TFF waliotoa mbegu za nyasi kwa ajili ya uwanja huo.
Akiwa
uwanjani hapo, Waziri Mkuu alipokea ahadi ya tani nne za nondo zenye
thamani ya sh. milioni 10, kutoka kwa Kampuni ya Hyseas International
Investment (T) Limited ya China.
Mapema,
akisoma taarifa ya ujenzi wa uwanja huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Afisa Utamaduni wa Wilaya hiyo, Bw.
Simon Mwambe alisema awamu ya kwanza ya ujenzi inatarajiwa kukamilika
Juni 2019 na hadi kukamilika kwake, uwanja huo utagharimu sh. bilioni
4.64.
Alisema
uwanja huo ambao unajengwa kwa kutumia vipimo vya kimataifa,
ukikamilika utawezesha watazamaji 10,500 kuingia uwanjani. Pia
utajumuisha michezo mingine kama mpira wa miguu, pete, wavu, mikono,
kikapu na riadha.
Naye
Architecture Khalid Yassin ambaye alikuwa akitoa maelezo ya ujenzi wa
uwanja huo kwa Waziri Mkuu, alisema utakapokamilika, uwanja huo utakuwa
na kumbi mbili za kukutania wachezaji na makocha wao, vyumba vya
kubadilishia, vyoo na ofisi ya meneja wa uwanja.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
