WANANDOA WASHIKILIWA KWA WIZI WA MTOTO WA SIKU MOJA WODINI
Shangwe na vilio vimetawala katika
Kata ya Iganzo jijini Mbeya baada ya mtoto wa kike wa siku moja
aliyeibwa katika wodi ya wazazi kupatikana akiwa hai.
Wanandoa Happy Charles (24) na Chiluba
Peter ambaye ni dereva wa teksi anayeegesha eneo la Hospitali ya Mkoa wa
Mbeya wanashikiliwa na Polisi wakituhumiwa kuhusika na wizi huo.
Februari Mosi, 2018 mwanamke
aliyejifanya muuguzi wa Hospitali hiyo aliingia katika wodi ya wazazi
na kumchukua mtoto wa Sarah Mwasanga (40) kwa madai ya kwenda kumpatia
chanjo.
Akizungumzia tukio hilo jana Februari
3, 2018 Kaimu Mganga Mkuu wa Hosptali hiyo, Yahaya Msuya amesema mara
baada ya tukio hilo mama wa mtoto huyo alitoa taarifa kwa uongozi wa
hospitali.
Amesema baada ya kupata taarifa hizo,
uongozi wa hosptali kwa kushirikiana na polisi na wananchi waliweka
mitego katika maeneo mbalimbali iliyowezesha kukamatwa watuhumiwa.
Msuya amesema mtuhumiwa alifika
hospitali ya mkoa akiwa katika pikipiki huku akiwa amebeba kitu mfano wa
mtoto na alipohojiwa na walinzi aliwaeleza kuwa ana mgonjwa
aliyeandikiwa sindano za masaa.
Amesema hali ya mtoto huyo inaendelea vizuri na yupo katika uangalizi wa madaktari kutokana na mazingira waliyomkuta baada ya kuibwa.
Mama wa mtoto huyo amesema, “Siamini
kilichotokea, nilitambua mwanagu amechukuliwa kimazingira na mwanamke
aliyefika katika wodi ya wazazi akiwa kama muuguzi kwa kweli yote
namwachia Mungu.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya,
Mohamed Mpinga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mpaka sasa
wanawashikiliwa wanandoa hao.
Amesema bado wanaendelea na taratibu za
kisheria za kuwahoji na watafikishwa mahakamani wakati wowote mara
baada ya uchunguzi kukamilika.
Na Hawa Mathias, Mwananchi