TUME YA UCHAGUZI YARIDHIA KUHAMISHWA KWA VITUO 46 VYA KUPIGIA KURA KINONDONI
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeridhia kuhamishwa kwa vituo 46 vya
kupigia Kura katika kata tatu za jimbo la Kinondoni zitakazofanya
Uchaguzi mdogo wa Ubunge Februari 17 mwaka huu.
Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw. Ramadhani Kailima ameeleza kuwa uamuzi wa NEC
kuridhia kuhamishwa kwa vituo hivyo, umetokana na makubaliano
yaliyofikiwa katika Mkutano wa Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo la
Kinondoni na Vyama vya siasa juu ya kuhamishwa kwa vituo hivyo
vilivyokuwa kwenye nyumba za Ibada, Zahanati na maeneo ya majengo ya
watu binafsi.
Amesema Tume imeridhika na uamuzi huo kwasababu hatua zilizochukuliwa ni
sahihi kwa mujibu sheria na kanuni namba 21 ya Uboreshaji wa Daftari la
Kudumu la Wapiga Kura ambayo inaeleza kuwa ; Vituo vya Kupigia Kura
havitakiwi kuwekwa katika majengo ya nyumba za Ibada, kambi za jeshi,
nyumba za watu binafsi na ofisi za vyama vya siasa.
“ Tumejiridhisha kuwa baadhi ya vituo katika Kata ya Kigogo vilikuwa
katika nyumba za Ibada na vingine kuwa katika maeneo yenye ufinyu wa
nafasi hivyo tumeridhia vituo hivyo vihamishwe na kupelekwa katika
majengo ya umma” Amesema.
Amesema kuwa baadhi ya vituo vya kupigia Kura vilivyokuwa katika majengo
ya umma ikiwemo Zahanati vimehamishwa katika shule za msingi za umma
zilizo katika kata hizo ili kuondoa usumbufu kwa wagonjwa.
Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Mwananyamala Bi. Barima Omari
ameeleza kuwa kata ya Mwananyamala ina vituo vya kupigia kura 65 na
wapiga kura 27,589 na kuongeza kuwa vituo nane (8) vilivyokuwa katika
shule ya Sekondari Kambangwa mtaa wa msisiri A vimehamishwa. Kati ya
hivyo 6 vimehamishiwa katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa ya Msolomi na 2
kuhamishiwa uwanja wa kwakopa.
Naye Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Kijitonyama Elizabeth Minga
ameeleza kuwa Kata hiyo ina jumla ya vituo vya kupigia Kura 101, kati
ya hivyo vituo 22 vimehamishwa.
Akifafanua kuhusu vituo hivyo amesema vituo 6 vilivyokuwa katika shule
ya Sekondari Kenton vimehamia shule ya Msingi Mapambano na vituo 5
vilivyokuwa nje ya Ofisi ya serikali ya Mtaa wa Bwawani vimehamishiwa
mbele ya ofisi hiyo.
Aidha, vituo 6 vilivyokuwa nje ya soko la Makumbusho vimehamia ndani ya
Ofisi ya Meneja wa Soko hilo na vituo 5 vilivyokuwa katika Ofisi ya
Serikali za mitaa kijitonyama vimehamishiwa katika shule ya msingi
kijitonyama.
Kwa upande wake Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Kata ya Kigogo Bw.
Singoro Mdegela ameeleza kuwa kata yake ina idadi ya Wapiga kura 27,000
na Vituo vya Kupigia Kura 59.
Amesema katika Kata hiyo vituo 16 vimehamishwa ambapo vituo 5
vilivyokuwa eneo la Kiwenge kwenye Msikiti wa Shiha vimehamia Uwanja wa
People na Vituo 6 vilivyokuwa kwenye Zahanati ya Kigogo vimehamishiwa
katika Shule ya Msingi Kigogo ili kuruhusu shughuli za matibabu kwa
wagonjwa kuendelea.
Aidha, vituo 5 katika ofisi ya serikali ya mtaa wa Mkwajuni vimehamishiwa katika shule ya secondari Kigogo.