SERIKALI KUGHARAMIA MAZISHI YA MWANAFUNZI ALIYEPIGWA RISASI NA POLISI DAR
Serikali imetoa pole kwa familia ya
mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline
aliyeuawa kwa kupigwa risasi Februari 16,2018 na kuahidi kugharamia
mazishi yake.
Akizungumza leo Februari 18,2018 na
vyombo vya habari, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce
Ndalichako amesema pamoja na katibu mkuu wa wizara watahakikisha
wanasimamia shughuli zote za msiba huo.
Amesema Akwilina alikuwa katika majukumu yake ya kawaida akipeleka barua yake ya mafunzo kwa vitendo Bagamoyo alipofariki dunia.
"Mafunzo yake kwa vitendo yalikuwa
yanatarajiwa kuanza Februari 26, mwaka huu, hivyo kifo chake kimeleta
simanzi kwa wananchi wote na Serikali kwa jumla.”
"Akwilina alikuwa ni miongoni mwa
wanafunzi wa kike waliojipambanua kwa kujua umuhimu wa elimu,
alihakikisha anasoma kwa bidii kwa manufaa yake na familia yake, lakini
pia alinufaika na mkopo wa elimu ya juu," amesema Profesa Ndalichako.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,
Hamad Masauni amesema uchunguzi wa tukio hilo utafanyika haraka
iwekezanavyo, kwa weledi na utaalamu ili haki itendeke.
"Tutafanya uchunguzi na kuwachukulia
hatua kali za kisheria wote watakaobainika kuhusika na tukio hilo,
Serikali tunasikitishwa na kifo cha mwanafunzi huyu, pia na kujeruhiwa
raia na askari polisi wawili," amesema Masauni.
Amesema Serikali haiwezi kuyaacha matukio hayo yapite kama yalivyo, hivyo imeyachukulia kwa uzito unaostahili.
Chanzo- Mwananchi
