Rais Magufuli: "Sitalalamika tena,najua nitakavyofanya"
Rais
John Magufuli amewapa pole Majaji kwa changamoto wanazokumbana nazo
pindi wanapo shughulikia mashitaka yanayopelekwa na serikali na kuahidi
kulifanyia kazi jambo hilo kabla ya mwezi Februari kuisha kwa madai
ameshajifunza vya kutosha.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo wakati alipohudhuria kilele cha maadhimisho ya 22 ya siku ya Sheria na uzinduzi wa mwaka mpya wa kimahakama yaliyofanyika jijini Dar es Salaam ambapo yeye binafsi ndio alikuwa mgeni rasmi katika shughuli hizo akiongozana na viongozi wengine wa serikali.
"Kwa
kuadhimisha siku hii ya sheria maana yake ni kwamba nchi yetu inatambua
umuhimu wa sheria katika kusimamia haki, kudumisha amani na kuleta
maendeleo ya nchi. Maadhimisho haya ya siku ya sheria ni muhimu kwa vile
yanatoa fursa kwa vyombo vinavyohusika na masuala ya sheria na utoaji
haki", alisema Rais Magufuli.
Aidha,
Rais Magufuli alisema bado kuna tatizo kubwa katika ofisi ya DPP
(Mkurugenzi wa Mashtaka) na AG (Mwanasheria Mkuu), na ndio maana muda
mwingine inawapelekea kuwapa changamoto kubwa Majaji.
"Najua
mnapata shida sana mnapo-dili na mashitaka yanayoletwa na serikali
mnauona kabisa ushahidi upo lakini watetezi hawajitokezi hadharani
kuutetea. Mwaka jana nililalamika lakini mwaka huu nitalishughulikia
vizuri. Sitalalamika tena ninajua nitakavyofanya kwa sababu
nimeshajifunza vya kutosha na nimejua wapi kuna 'weakness' na wala huu
mwezi wa Februari hautoisha", alisisitiza Rais Magufuli.
Kwa
upande mwingine, Rais Magufuli amewataka viongozi wengine wanaosimamia
vyombo vya sheria kufuata mfano mzuri aliyouanzisha Profesa Ibrahimu
Juma kwa kutowafumbia macho wahalifu wa aina yeyote ile.