Rais Magufuli Amtumbua Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Rais
Magufuli amefanya uteuzi mpya kwa kumteua Dk Adelardus Kilangi kuwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Paul Ngwembe kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu
wa Serikali.
Taarifa
iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, imeeleza kuwa
Rais Magufuli pia amewateua aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali
George Masaju na Naibu wake, Gerson Mdemu kuwa Majaji wa Mahakama Kuu,
kuanzia leo.
Kabla
ya uteuzi, Dk Kilangi alikuwa Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu
Agustino (St.Augustine University) kituo cha Arusha, na pia ni
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu
wa Mafuta, (Tanzania Petroleum Upstream Regulatory Authority- PURA).
Taarifa
ya Ikulu imeeleza pia kuwa, Naibu Mwanasheria Mkuu Paul Ngwembe kabla
ya uteuzi, alikuwa Mkurugenzi wa masuala ya sheria katika Mamlaka ya
Usimamizi wa Bima Tanzania (Tanzania Insurance Regulatory
Authority-TIRA).
Wateule wote wanatarajiwa kuapishwa Jumamosi asubuhi tarehe 3 Februari 2018.
Awali
katika maadhimisho ya Siku ya Sheria, yaliyofanyika jijini Dar es
Salaam, Rais Magufuli katika hotuba yake, aliwanyooshea vidole Waziri wa
Katiba na Sheria, Prof Palamagamba Kabudi, na aliyekuwa Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, George Masaju na Naibu wake Gerson Mdemu wameshindwa
kuandaa kanuni za msaada wa kisheria.
Rais
Magufuli alitoa mwezi mmoja kwa viongozi hao, kukamilisha kanuni za
msaada wa kisheria, huku akiongeza kuwa usimamizi wa sheria na utoaji
wa haki, bado una changamoto, kwani wapo wachache, uadilifu wao na
matendo yao yanachafua vyombo nyeti.