Dokta Mpango Ateta Na Mkurugenzi Mtendaji Wa Benki Ya Barclays Kuhusu Reli Ya Kisasa Na Mradi Wa Umeme Wa Stiegler's Gorge
Benny Mwaipaja, Dodoma
Waziri
wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, amekutana na Naibu Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya Barclays Kanda ya Afrika, Bw. Peter Matlare na
kuiomba Benki hiyo kuangalia uwezekano wa kutoa mkopo nafuu wa ujenzi wa
miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali ukiwemo ujenzi wa Reli ya
Kati kwa viwango vya kimataifa (SGR) mradi wa miundombinu ya umeme wa
Stieglar's Gorge ili kurahakisha maendeleo ya kiuchumi kupitia viwanda.
Amemweleza
kiongozi huyo kwamba Serikali imeimarisha uchumi Mkuu kwa kudhibiti
mfumuko wa bei ambao uko katika kiwango chatarakimu moja cha wastani wa
asilimi 5.3 katika kipindi cha miezi 6 iliyopita.
"Tumewekeza
kwenye miundombinu kama vile Elimu, maji, kilimo, afya, madini, na
biashara na kwamba katika kipindi kifupi cha miaka 2 zaidi ya viwanda 80
vimejengwa katika eneo la Mkuranga mkoani Pwani, kutokana na fursa za
uwepo wa bomba la gesi na eneo hilo kuwa karibu na Bandari ya Dar es
Salaam.
Dkt.
Mpango ameelezea pia mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha
Kimataifa (SGR) ambao amesema utarahisisha usafiri na usafirishaji wa
abiria na mizigo katika nchi zinazopakana na Tanzania hivyo kukuza
biashara kwa kiwango kikubwa.
Akizungumzia
kuhusu ujenzi wa mradi mkubwa wa umeme katika Bonde la mto Rufiji
(Stiegler's Gorge), Dkt. Mpango amesema lengo la mradi huo utakao
zalisha megawati 2,100 za umeme utakao kuwa wa uhakika na bei nafuu ili
kukuza viwanda.
Alisema
kuwa mwelekeo wa Serikali kwa sasa ni kuhakikisha kuwa kila biadhaa
zinazozalishwa nchini pamoja na madini, vinaongezwa thamani hapa hapa
nchini badala ya kuuzwa kama malighafi na kwamba nishati ya umeme ndiyo
nguzo kuu ya kufikia malengo hayo.
"Ili
tuweze kufikia azma hiyo tunahitaji kuwa na umeme wa uhakika na wa bei
nafuu ili viwanda vyetu viweze kuzalisha kwa wingi ndio maana tunaiomba
Benki yako iweze kufikiria namna ya kushiriki katika ujenzi wa miradi
hii" Alisisitiza Dkt. Mpango.
Dkt.
Mpango ameipongeza Benki ya Barclays ambayo pia ni mwanahisa katika
Benki ya NBC kwa ahadi yake ya kutaka kuwekeza kiteknolojia katika sekta
ya benki nchini hatua ambayo itasaidia kukuza mitaji na mikopo kwa
kundi kubwa la watanzania wakiwemo wajasiriamali wadogo, wa kati na
wakubwa.
Alielezea
msimamo wake kwamba katika kukuza uchumi, Serikali inathamini mchango
mkubwa wa Sekta Binafsi na imeendelea kuweka mazingira mazuri ya
uwekezaji na kwamba hivi karibuni alikuta na wadau wa Sekta ya Benki ili
kusikiliza changamoto zao na pia kuwaeleza mambo muhimu ambayo
ingependa sekta Binafsi ifanye ili kufikia malengo yanayokusudiwa.
Awali,
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo ya Barclays anaye hudumia kundi
la benki za Barclays Barani Afrika na kwingineko Marekani na Ulaya, Bw.
Peter Matlare, ameipongeza Serikali chini ya Rais Dkt. John Magufuli
kwa kusimamia kikamilifu uchumi wa nchi unaokua kwa wastani wa asilimia
7.
Alisema
hatua hiyo ni ya kupigiwa mfano katika nchi za Kiafrika na Duniani kwa
ujumla ambapo amesema Tanzania imekuwa ikifanya vyema katika kukuza
uchumi jumuishi unaowafikia watu wengi zaidi wakiwemo waishio mijini na
vijijini.
Bw.
Peter Matlare amemhakikishia Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip
Mpango, kwamba Benki yake itayafanyia kazi mapendekezo ya kutaka
ushiriki wake katika ujenzi wa miradi mikubwa iliyoainishwa na Serikali
kuwa kipaumbele chake.
Mwisho