JUKWAA LA NISHATI TANZANIA KUTOA SEMINA KWA WABUNGE
JUKWAA la Nishati Tanzania linatarajia
kutoa semina kwa wabunge ili wapate uelewa wa nishati na changamoto
zake, watakapokuwa wanajibu maswali ama kuuliza wafanye hivyo kwa
manufaa ya taifa.
Mratibu wa Jukwaa hilo nchini ambaye ni
mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Hudson Nkotagu
alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
shughuli wanazozifanya.
Profesa Nkotagu alisema wanaamini
wabunge wakipata uelewa kuhusu nishati pale watakapokuwa wakijadili
masuala hayo bungeni watakuwa na uelewa mpana, na maamuzi yake yatakuwa
kwa manufaa ya taifa.
Pia alisema semina hizo zitatolewa kwa
viongozi wakuu, watendaji wa serikali kutoka sekta za viwanda,
mazingira, serikali za mitaa, wawekezaji pamoja na wafanya biashara
mbalimbali.
Alisisitiza kuwa wananchi wengi hawana
uelewa wa nishati kwamba kuna za aina mbili, aina ya kwanza inatokana na
vyanzo vya nishata ambavyo vikitumika vinapoisha havirudi tena mfano
gesi, mafuta, mkaa wa mawe pamoja na urani.
Na aina nyingine ni ile inayotokana na
vitu ambavyo vinajiendeleza vyenyewe kiasili kwa mfano nishati ya sola,
upepo, maji, mawimbi ya bahari na kuni.
“Nishati hizi zinajiendeleza kiasili.
Kwa bahati nzuri zote tunazo katika nchi yetu. Tanzania imejaliwa kuwa
na vyanzo vyote vya nishati, vinahitajika tu kuendelezwa,” alisema.
Alisema jukwaa hilo linashirikisha UDSM,
Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), Taasisi ya Sayansi na
Teknolojia ya Karume (KIST), pamoja na vyuo vikuu vine kutoka nchini
Uholanzi ambavyo ni Twente, Ultreacht, Hanze na Delft.
