AG mpya aahidi makubwa sekta ya sheria
Na Fatma Salum-MAELEZO
Mwanasheria
Mkuu wa Serikali Dkt. Adelardus Kilangi ameahidi kufanya kazi kwa bidii
ili kupunguza changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya Sheria hapa
nchini.
Akizungumza
baada ya kuapishwa katika hafla iliyofanyika jana ikulu jijini Dar es
Salaam, Dkt. Kilangi alisema kuwa changamoto hizo haziishii katika ngazi
ya kitaifa tu bali hata kwenye nchi nyingine za Afrika na Jumuiya za
Kimataifa.
“Natambua
kuwa yapo mambo mengi yanahitaji kufanyiwa kazi na kila nchi katika
Afrika ikiwemo Sheria za udhibiti wa rasilimali zetu na mfumo wa Sheria
za Kimataifa unaohusu masuala ya uwekezaji,” alisisitiza Kilangi.
Kilangi
aliongeza kuwa atahakikisha ofisi yake inazishughulikia kwa karibu
changamoto hizo kwa kushirikiana vyema na wadau wengine wa sheria ili
kuongeza ufanisi katika Serikali kwa maslahi ya taifa.
“Tunakuahidi
Mhe. Rais kwamba tutafanya kazi kwa akili zetu zote, nguvu zetu zote na
uwezo wetu wote kwa maslahi ya Watanzania,” alisema Kilangi.
Kwa
upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma aliwapongeza
majaji wapya walioapishwa katika hafla hiyo na kuwaeleza kuwa nafasi ya
Majaji wa Mahakama Kuu ni muhimu sana katika taifa hivyo ni wajibu wao
kufanya kazi na kufuata sheria bila upendeleo.
Naye
Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi alibainisha kuwa
mabadiliko aliyofanya Mhe. Rais ya kuwateua Mwanasheria Mkuu wa Serikali
na Naibu wake ni mwanzo tu wa mabadiliko makubwa ambayo amedhamiria
kuyafanya katika Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali.
Alieleza
kuwa lengo la mabadiliko hayo yanayotekelezwa na Rais John Magufuli ni
kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi.
“Namuomba
Mhe. Rais taratibu zifanyike ili wanasheria wote walioko katika wizara
zote za Serikali Kuu warudi chini ya usimamizi wa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ili kuimarisha uwezo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
na kuongeza ufanisi,” alisema Kabudi.
Akitoa
nasaha zake kwa wateule walioapishwa kwenye hafla hiyo, Naibu Spika wa
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson aliwaasa
kutofanya kazi kwa mazowea kwa kuwa yapo mambo mengi yanahitaji
maboresho ikizingatiwa kwamba ulimwengu unabadilika kwa kasi kubwa.
Aidha,
aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju ambaye uteuzi wake
ulitenguliwa katikati ya wiki hii ameapishwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu
ya Tanzania na kuahidi kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano katika
kuwatumikia wananchi na taifa kwa ujumla.
Katika
hafla hiyo iliyohusisha kiapo cha utii na kiapo cha maadili
walioapishwa ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Adelardus
Kilangi , Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Paul Ngwembe na Majaji
wawili wa Mahakama Kuu ambao ni George Masaju na Gerson Mdemu.
Kabla
ya uteuzi, Dkt. Adelardus Kilangi alikuwa Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha
Mtakatifu Agustino (SAUT) kituo cha Arusha na Paul Ngwembe alikuwa
Mkurugenzi wa masuala ya Sheria katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bima
Tanzania (TIRA).