Viwanda Vitano vya Samaki Vyapigwa Faini ya Milioni 180 na Wanakiwa Kuilipa Ndani ya Masaa 24
WAZIRI
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amewaamuru wamiliki wa viwanda vitano
vya kuchakata minofu ya samaki vilivyoko jijini Mwanza kulipa faini ya
shilingi milioni 180 ndani ya saa 24 baada ya kubainika kupokea na
kuchakata samaki wasioruhusiwa kwa kukiuka Sheria ya Uvuvi namba 22 ya
mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009 sambamba na Sheria ya usimamizi
wa Mazingira namba 20 ya mwaka 2004
Pia Waziri Mpina amechukizwa na kitendo cha viwanda hivyo kufadhili uvuvi haramu na kueleza kuwa ni bora kutokuwa na kiwanda hata kimoja cha samaki kuliko kuendelea kuwa na viwanda vinavyofadhili uvuvi haramu na kutishia kuvifunga viwanda vyote sambamba na kutaifisha samaki, magari na boti zinazobeba samaki wasioruhusiwa.
Waziri
Mpina amesema hayo jana kwa nyakati tofauti wakati alipofanya ziara
kutembelea viwanda vinavyochakata samaki jijini Mwanza ambapo pia
alimuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Yohana Budeba
kuwasimamisha kazi maofisa watatu wa Kitengo cha Udhibiti wa Usalama na
Ubora wa Mazao ya Uvuvi Kituo cha Mwanza kutoka Wizara ya Mifugo na
Uvuvi kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria na
kulisababishia Taifa hasara kubwa.
Maofisa
hao ambao Waziri Mpina ameagiza wasimamishwe kazi na kuchukuliwa hatua
kali za kinidhamu ni pamoja na Philemon Mugabo,Dorina Mlenge na John
Bosco Rubajuna
Waziri
Mpina ametaja viwanda vilivyokutwa vikichakata samaki wasioruhusiwa
wakiwemo samaki wazazi na samaki wachanga na idadi ya kilo
zilizokamatwa kwenye mabano kuwa ni pamoja na Nile Perch Fish (920),
Victoria Fish (131), Nature Fish (150), Omega Fish (580), Tanzania Fish
Processing (842) huku magari 41, boti 15, Nyavu haramu 294 wakiwa na
samaki wachanga na wazazi ambapo sheria inakataza kuvuliwa samaki chini
sentimita 50 na juu ya sentimita 85 .
Majina
ya viwanda hivyo na faini zao walizotozwa Nile Perch sh milioni 25,
Tanzania Fish Processing sh. milioni 50, Victoria Perch Milioni 30,
Nature Fish milioni 25, Omega Fish Ltd milioni 50 ambapo amesisitiza
kuwa adhabu hiyo ni ya kwanza na ya mwisho na kwamba ikithibika tena
wenye viwanda waendelea kufadhili uvuvi haramu hatua za kuvifunga
viwanda na kutaifisha mali ikiwemo mitumbwi, boti na magari yatakayokuwa
yanabeba samaki hao itafuata.
Waziri
Mpina amesema ukanda wa Ziwa Victoria ulikuwa na Viwanda 13 vya
kuchakata samaki vilivyokuwa na uwezo wa kuchakata tani 1,065 kwa siku
lakini kutokana na kushamiri kwa uvuvi usiongatia sheria kumesababisha
viwanda 5 kufa kutokana na kukosekana malighafi na kwamba viwanda 8
vilivyobaki sasa vinachakata tani 171 tu kwa siku huku ajira zikiwa
zimeporomoka kutoka ajira 4, 088 na kufikia 2,179 tu.
Mpina
amesema tayari Rais Dk John Magufuli ameshatoa maagizo kwa wavuvi
kuachana na uvuvi haramu sambamba na wenye viwanda kutofadhili uvuvi huo
huku pia Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan naye akisisitiza jambo
hilo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikikemea vikali huku Sheria za nchi
nazo zikikataza jambo hilo lakini wenye viwanda kwa makusudi wameamua
kudharau maagizo ya viongozi wakuu wa nchi jambo ambalo Wizara ya Mifugo
na Uvuvi chini ya uongozi wake Waziri Mpina haliwezi kukubalika kamwe.
Katibu
Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dk. Yohana Budeba amesema kama
watumishi wa wizara yake wangesimamia majukumu yao kikamilifu mambo hayo
aliyobaini Waziri Mpina yasingejitokeza huku akikiri kupokea maagizo
yake yote na atayasimamia kwa haraka kuona yanatekelezwa.
Afisa
Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa
Mazingira(NEMC), Mhandisi Boniphace Guni amesema wenye viwanda hivyo
wamekutwa na makosa ya kupatikana na samaki waliochini wa ukubwa,
kukutwa na samaki wachanga kinyume cha Sheria ya Usimamizi Mazingira
namba 20 ya mwaka 2004 pamoja na Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003
ambapo wamekiuka kifungu namba 58(I)(a) hivyo wamestahili adhabu hiyo
ya kulipa faini ya milioni 180 ndani ya saa 24
Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina akimbeba samaki aina ya sangara
aliyevuliwa kinyume na taratibu alipokuwa katika ukaguzi wa mazao ya
uvuvi katika Kiwanda cha Nature Fisheries Limited Jijini Mwanza, kushoto
ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt Yohana Budeba na kulia ni Afisa Uvuvi
Mkuu Bw. Boniface Shatila.
Samaki
mzazi aina ya Sangara aliyevuliwa kinyume na taratibu(alikuwa na urefu
wa sentimita 120), samaki ambaye akiachwa ziwani kwa muda wa miezi
mitatu ana uwezo wa kuzaa samaki milioni tatu, na kuongeza idadi kubwa
ya jamii
hiyo ya samaki katika ziwa Victoria.
hiyo ya samaki katika ziwa Victoria.
Samaki chini ya sentimita 50 na mwenye zaidi ya sentimita 85 hawaruhusiwi kisheria kuvuliwa.