Ujenzi wa reli ya kisasa watarajiwa kuanza Machi mwaka huu
Serikali
imesema ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge) kutoka Morogoro hadi
Makutopora mkoani Dodoma ambao utaanza kabla ya Machi mwaka huu,
utagharimu dola 1.923bilioni za kimarekani (sawa na Sh4.3 trilioni).
Meneja
Mradi huo wa Kampuni Hodhi ya Raslimali za Reli (Rahco) Mhandisi Maizo
Mgedzi amesema mradi huo unatarajia kuanza wakati wowote kabla ya Machi.
Amesema
treni hiyo ina uwezo wa kwenda kilometa 160 kwa saa itahifadhi
mazingira na kwamba itaweza kubeba mzigo mkubwa kwa zaidi ya mara tano
ya reli ya sasa.
“Pia itaweza kubeba watu na mizigo kwa usalama kwa maana hakutakuwa na ajali zinazosababishwa na ubovu wa miundombinu,” amesema
Meneja
wa Kampuni ya Yapi Merkezi iliyopewa zabuni ya mradi huo, Abdullah
Kilic amesema kuwa jiwe la msingi la mradi huo litawekwa wakati wowote
kuanzia sasa.
“Tunachosubiri ni utaratibu wa Ikulu lakini jiwe la msingi tutaliweka wakati wowote kuanzia sasa,”amesema.
Mbunge
wa jimbo la Dodoma Mjini, Antony Mavunde amesema Serikali ingependa
mradi huo ulete matokeo chanya kwa watu wa Dodoma na si laana.
“Matokeo
haya yasiwe laana kwa maana tusije kuiacha reli hii ipite tu hapana.
Sisi tunataka kwa watu wa Dodoma reli hii iwe kichocheo cha kwanza cha
uchumi ikiwezekana kubadilisha mji,”amesema.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,
Deogratius Ndejembi amesema viongozi watawapa ushirikiano wa kutosha
katika kipindi cha miaka mitatu cha ujenzi wa reli hiyo na kurekebishana
kwa baadhi ya mambo.
“Wamesema
asilimia 80 (watu 3000) watachukua watu wa Dodoma kwa hiyo ni jambo
kubwa sana. Hii ni fursa kubwa hata kipindi hiki cha ujenzi,”amesema.