Madiwani Watatu wa CHADEMA Kilimanjaro Watimkia CCM
Katika
Kikao cha Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Rombo, Katibu wa NEC Mwenye
dhamana ya Itikadi na Uenezi Ndg. Humphrey Polepole ameujulisha umma wa
wananchi wa Rombo kuwa baada ya ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani na
kutambua uwepo wa kero kubwa ya Maji, amewasiliana na Uongozi wa Wizara
ya Maji na Umwagiliaji na kwamba ukosefu wa kiasi cha shilingi Milioni
130 kilichokuwa kinakosekana ili kufanya upembuzi yakinifu wa mradi wa
kuvuta maji kutoka Ziwa Chala sasa zitatolewa na Wizara ili tatizo la
upungufu mkubwa wa maji Wilaya ya Rombo limalizike.
Aidha
Ndg. Polepole akawaelekeza watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo
kufanya mawasiliano ya haraka na Wizara ya Maji na Umwagiliaji ili
kupata fedha hizo na kuhakikisha mchakato wa kuvuta maji kutoka Ziwa
Chala unaanza maramoja.
Wakati
Kikao Cha Halmashauri Kuu ya Wilaya na Katibu wa Nec Itikadi na Uenezi
kikiendelea madiwani watatu wa Chadema walifika eneo la kikao na kuomba
wapewe fursa ya kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Pamoja na maelezo
waliyoyatoa Madiwani hao wa Chadema katika kikao Cha Halmashauri Kuu ya
Wilaya juu ya sababu zilizopelekea kujitoa kwao Chadema na kujiunga na
CCM, wameelezea pia siri ya kudorora kwa Maendeleo Wilaya ya Rombo kuwa
ni mpasuko uliopo kati ya Madiwani wanaomwunga mkono Mbunge wa Jimbo la
Rombo Ndg. Joseph Selasini na madiwani wanaomwunga mkono Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya ya Rombo Ndg. Evarist Silayo sababu ikiwa ni vita
ya Ubunge mwaka 2020.
Kikao
cha Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Rombo kwa kauli moja wamewapokea
wanachama hao wapya na Ndg. Polepole akaelekeza uongozi wa Wilaya
kuwapitisha katika program ya mafunzo ya Imani, Itikadi, Siasa, Masharti
ya Mwanachama, Ahadi za Mwanachama na Sera za Maendeleo za CCM.
Madiwani
waliojitoa CHADEMA na kujiunga na CCM leo ni Ndg. Juliana Malamsha na
Martha Ushaki wa Viti Maalum pamoja na Frank Lubega wa kata ya
Kelamfuamokala.
Huu
ni muendelezo wa ziara za ujenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika
kuhuisha dhana ya Chama kushika hatamu na kuhakikisha kinaisimia
Serikali katika kushughulika na shida za wananchi.
Imetolewa na,
IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM), ROMBO, KILIMANJARO