Nabii Tito Ajaribu Kujiua....Ashonwa Nyuzi 25
Siku
mbili baada ya kukamatwa na polisi kwa mahojiano kwa Tito Machibya,
maarufu Nabii Tito, anadaiwa kujaribu kujiua kwa kujikata na wembe
tumboni na kushonwa nyuzi 25.
Nabii
Tito alikamatwa na polisi mkoani Dodoma kwa kosa la kufundisha
mafundisho yaliyo kinyume na dini kwa kuhamasisha watu kunywa pombe
kwani si dhambi na kuoa wafanyakazi wao wa ndani ambapo hata hivyo,
jeshi hilo lilisema nabii huyo ana matatizo na akili yaliyothibitishwa
na daktari wa Hospitali ya vichaa ya Milembe mkoani Dodoma.
Inadaiwa
kuwa, jana polisi waliambatana na nabii huyo nyumbani kwake Ng’ong’ona
mkoani humo kwa ajili ya upekuzi ambapo aliingia ndani na kutoka akiwa
anavuja damu tumboni huku ameshikilia wembe mkononi ambapo iliwalazimu
polisi hao kumkimbiza Zahanati ya Polisi ya Mkoa wa Dodoma.
Mmoja
wa madaktari wa zahanati hiyo kwa sharti la kutotajwa jina amesema
nabii huyo alifikishwa, saa tisa alasiri akiwa na jeraha kubwa tumboni.
“Alifikishwa
na kushonwa nyuzi 25 na kuruhusiwa kwani hakuwa na shida nyingine
yoyote halafu jeraha lake halikufunguka kwa ndani sana, kwa hiyo
hakutoka damu nyingi sana alitibiwa na kuondoka na askari.
Kamanda wa Polisi Mkoani Dodoma, Gilles Muroto alipoulizwa kuhusu tukio hilo hilo alisema hana taarifa.
Chanzo: Mtanzania