Waziri Mkuu Awaasa Watendaji Wa Taasisi Zinazosimamia Mazao Ya Biashara
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa taasisi zilizopewa dhamana
ya kusimamia mazao makuu matano ya biashara ambayo ni ya pamba, tumbaku,
korosho, chai na kahawa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Amesema
mazao hayo ni muhimu sana katika kuwezesha mkakati wa Serikali ya Awamu
ya Tano wa kufikia uchumi wa viwanda kwani ndiyo mhimili wa kutoa
malighafi za kuendesha viwanda husika na yana mnyororo mpana wa
uzalishaji ambao una fursa ya kutoa ajira nyingi.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Ijumaa, Septemba 15, 2017) Bungeni mjini
Dodoma alipowasilisha hotuba yake ya kuahirisha Mkutano wa Nane wa
Bunge. Amesema Serikali imejipanga kuimarisha usimamizi katika
uzalishaji na uuzaji wa mazao hayo.
Alisema
Serikali itahakikisha kuwa kila taasisi iliyopewa dhamana ya kusimamia
mazao hayo, inatekeleza majukumu yake ipasavyo sambamba na kuhakikisha
kwamba Watendaji wake wanafanya kazi hiyo kwa uadilifu na ufanisi
mkubwa.
Alisema
jitihada hizo zinalenga kuwawezesha wakulima wengi hususan wa vijijini
ambao ni takriban asilimia 75 ya Watanzania wote, kulima kilimo cha
kisasa, chenye tija na cha kibiashara, hivyo kuondokana na umaskini wa
kipato.
“Vilevile,
kuwawezesha wakulima kupata mbinu za kisasa za kuyafikia masoko ya
uhakika ya mazao yao ili kupata bei nzuri ambayo itawakwamua kiuchumi.
Mazao mengine ya kibiashara yatakayotiliwa mkazo ni katani, ufuta,
alizeti, mbaazi na ngano.”
Alisema
kwa kipindi kirefu uzalishaji wa mazao hayo ulishuka kulitokana na
changamoto mbalimbali ikiwemo ya baadhi ya viongozi wa vyama vya
Ushirika kushindwa kutekeleza vyema wajibu wao, wizi, dhuluma kwa
wakulima na pia ushiriki mdogo wa Maofisa Kilimo katika kusimamia kilimo
cha kitaalam.
Wakati
huo huo, Waziri Mkuu amesema jumla ya vijana 1,000,000 wamelengwa
kupata urasimishaji ujuzi kati ya mwaka 2017 na 2021 kupitia Mpango wa
Kutathmini na Kurasimisha Ujuzi uliopatikana nje ya Mfumo Rasmi wa
Mafunzo.
Alisea
Serikali imeamua kuchukua hatua hiyo ili kuwawezesha vijana ambao ndiyo
nguvu kazi wachangie kikamilifu katika kujenga uchumi wa Taifa. “Hadi
sasa tayari vijana wengi wanaendelea kunufaika na mpango huu kutoka
mikoa mbalimbali.”
Miongoni
mwa faida za mpango huo ni pamoja na kuwasaidia mafundi waliojifunza
kupitia sehemu za kazi kupata kazi zenye staha na kuwajengea uwezo wa
kushiriki na kushindana kikamilifu katika soko la ajira. Pia kuinua tija
mahali pa kazi na kusaidia waajiri/wenye makampuni kukidhi viwango
katika eneo la rasilimali watu.
Waziri
Mkuu alisema mpango huu unafadhiliwa kwa asilimia 100 na Serikali na
unatekelezwa kwa pamoja na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (
VETA)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,