UWEKEZAJI MOROGORO WAWAWEKA MATATANI RAIA WATATU WA CHINA
Siku
moja baada ya agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutoa agizo kwa
uongozi wa Mkoa wa Morogoro kufuatilia utendaji wa kampuni ya Zhong
Fenq, umeviagiza vyombo vya ulinzi kuwakamata raia watatu wa China
wanaodaiwa kuendesha shughuli za uwekezaji kinyume cha sheria.
Juzi,
Waziri Mkuu Majaliwa alimuagiza mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen
Kebwe na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa kwenda katika kijiji cha
Maseyu kufuatilia utendaji wa kampuni hiyo kama inafuata sheria, kanuni
na utaratibu.
Dk
Kebwe jana alitoa agizo kwa vyombo vya ulinzi kuwakamata raia hao na
kuamuru warudishwe kwao mara moja baada ya kugundulika kujihusisha na
uchimbaji wa madini ya kutengeneza marumaru bila kufuata utaratibu,
kanuni na sheria za nchi.
Waziri
mkuu alitoa agizo hilo kutokana na malalamiko ya mbunge wa Morogoro
Kusini Mashariki, Omary Mgumba kuwa wawekezaji hao kutoka China
wanaendesha shughuli za uchimbaji bila ya kuwa na kibali.
Mgumba
alisema tangu mwaka 2011 wawekezaji hao wameendesha shughuli zao bila
kulipa kodi za Serikali na tozo za halmashauri, hivyo kuikosesha
Serikali mapato.
Mbunge huyo ambaye machimbo hayo yako jimboni kwake,
alisema
licha ya uongozi wa mkoa kwenda eneo hilo na kuizuia kampuni kuendelea
na uchimbaji hadi itakapopata vibali ilikaidi na kuendelea na shughuli
zake.
Majaliwa
alisema iwapo wahusika watabainika kuwa hawajafuata sheria, kanuni na
utaratibu hatua zichukuliwe dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuwaondoa
katika eneo hilo chini ya ulinzi na kuwasiliana na ubalozi wa China
nchini.
Akitoa
agizo jana, Dk Kebwe alimtaka kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro na
kamanda wa Uhamiaji wa mkoa kuhakikisha wanawakamata na kuwasafirisha
raia hao wa China hadi jijini Dar es Salaam na utaratibu wa kuwaondoa
nchini ufanyike mara moja.
“Nawaagiza kuhakikisha mnaorodhesha vifaa na vitu vyote vilivyopo katika mgodi huo,” alisema Dk Kebwe.
Raia
hao wa China kwa sasa wanashikiliwa na polisi wakisubiri kukamilishwa
kwa utaratibu wa kuwarudisha kwao, huku mali za mgodi huo zikiwa chini
ya uangalizi wa jeshi hilo.
Katika
hatua nyingine, Dk Kebwe aliagiza polisi kuwakamata mhasibu wa
halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, ofisa biashara, mtendaji wa kata ya
Maseyu na mtendaji wa kijiji hicho kwa kushindwa kutoa taarifa za raia
hao wa kigeni kuendelea na uchimbaji huo.
Pia, Dk Kebwe alisema waliendelea kuwatoza kodi ya huduma hadi Juni mwaka huu licha ya kujua kuwa hawana kibali.
Akizungumzia
kuchelewa kuondoka kwa Wachina hao, ofisa madini mkazi Mkoa wa
Morogoro, Bertha Luzabiko alisema mamlaka ya Wizara ya Nishati na Madini
ndiyo ilikuwa ikishughulikia suala lao.
Mkuu
wa uhamiaji Mkoa wa Morogoro, Safina Muhindi alisema mpaka sasa hajaona
pasipoti wala vibali vya kufanya kazi nchini vya rais hao, hivyo
ufuatiliaji unaendelea.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema walichofanya ni kutekeleza agizo la mkuu wa mkoa la kuwakamata
Mwaka
2016 mgodi huo ulizuiwa kufanya shughuli za uchimbaji wa madini na
uzalishaji wa marumaru baada ya kubainika kuwa wawekezaji hao hawana
vibali, huku bidhaa zilizokuwa zikizalishwa na kampuni hiyo zimekuwa
zikiandikwa kuwa zinatengenezwa China.
Imeelezwa uongozi wa mgodi ulisitisha shughuli kwa muda na baadaye ulirejea kuendelea na uzalishaji.