MTOTO MCHANGA AKUTWA AMEKUFA KWENYE MFEREJI WA MAJI MACHAFU
Mwili wa mtoto ambaye anakadiriwa kuwa na umri wa siku moja umeokotwa
kwenye mfereji wa kupitisha maji machafu katika eneo la Mtaa wa Ali
Nyanya kata ya Ungalimited jijini Arusha.
Kichanga hicho kimeonekana kutekelezwa na mama yake mzazi mara tu baada
ya kujifungua na kupelekea kupoteza maisha, baadhi ya wananchi wa eneo
hilo wamelaani kitendo hicho cha kinyama na kikatili kinachofanywa na
baadhi ya wanawake wasiokuwa na hofu ya Mungu ndani yao ambao
wanakatisha uhai wa watoto hao ambao hawana hatia.
Mwenyekiti wa Mtaa huo Omari Shehe naye amelaani kitendo hicho na
kuahidi kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha wanamtafuta muhisika
ambaye amefanya tukio hilo la kinyama ili iwe fundisho kwa watu wengine
wenye tabia hizo za kufanya uovu na ukatili huo.
Vitendo vya watu kutekeleza watoto vimekuwa vikishamiri katika maeneo
mbalimbali ya nchi huku wengi wakionekana kufanya ukatili huo kutokana
na baadhi ya wanaume kukataa watoto au ujazito jambo ambalo hata hivyo
halikubaliki.