Jeshi la Polisi Makao Makuu na TCRA Wazungumzia Makosa ya Mtandaoni na Hatua Ambazo Mwananchi Anatakiwa Kuchukua
Msemaji
wa Jeshi la Polisi nchini Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) Barnabas
Mwakalukwa amewataka wananchi kwa ujumla wanaofanyiwa vitendo vya
uhalifu mitandaoni wasiende TCRA bali wanapaswa kutoa taarifa katika
jeshi la polisi.
ACP
Mwakalukwa amebainisha hayo wakati alipokuwa anazungumza katika mkutano
wa pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuhusu suala zima
la uhalifu wa makosa ya mitandao ambapo kwa sasa limeshika kasi kubwa
"Chochote
kinachofanyika ambacho ni kosa jinai nawaomba msiende Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA), kwa watoa huduma wa mitandao ya simu
mbalimbali wala katika vyombo vya kutolea habari bali unapaswa uje
katika kituo cha polisi utoe taarifa zako kama ni kosa la jinai kwa
sababu mkienda huko uchunguzi utakuwa shida kwa maana wewe mwenyewe
utaweza kusababisha hata yule aliyekutendea uhalifu atoroke", amesema
ACP Mwakalukwa na kuongeza;
"Kutokana
na kukua kwa teknolojia vitu vingi vimekuwa vikifanyika 'online' kwa
hiyo hii mitandao ya kijamii imeonekana ni muhimu sana kwenye maendeleo,
lakini pia imebadilisha mbinu ya kufanya uhalifu katika mitandao ya
kijamii kwa kutumiwa na baadhi ya watu kutapeli, hata kutishia kuua,
hivyo jeshi la polisi limejipanga kwa ajili ya kushughulikia makosa
ambayo yanatokana na mtandao", amesema Mwakalukwa.
Kwa
upande wake,Kaimu Mkurugenzi wa TCRA, Thadayo Ringo amesema
analishukuru jeshi la polisi kwa kuweza kuwasaidia katika kuwatatulia
changamoto mbalimbali hasa za kiusalama huku akiwataka wananchi
watakaopata matatizo katika mtandao kwenda kutoa taarifa polisi ili
waweze kuwasaidia kabla ya kufika kwao.