Uamuzi pingamizi kesi ya Wema Sepetu kutolewa Agosti 31
Uamuzi
wa kupokea au kutopokea kielelezo cha ushahidi cha msokoto mmoja wa
bangi na vipisi viwili vya bangi katika kesi inayomkabili mlimbwende wa
Tanzania 2006, Wema Sepetu utatolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
mwisho wa mwezi huu.
Hakimu
Mkazi Mkuu,Thomas Simba amesema uamuzi huo ulipaswa autoe jana, lakini
bado kuna tafiti anazifanya, hajakamilisha hivyo aliuahirisha hadi
Agosti 31,2017.
Hata
hivyo, baada ya kutolewa kwa uamuzi huo shahidi wa kwanza wa upande wa
mashtaka ataendelea kutoa ushahidi wake katika kesi hiyo. Kesi hiyo
itaendelea kusikilizwa Septemba 12 na 13, 2017.
Uamuzi
huo umefuatia baada ya shahidi huyo ambaye ni mkemia kutoka ofisi ya
Mkemia Mkuu wa Serikali, Elias Mulima ambaye alipima msokoto mmoja na
vipisi viwili vinavyodaiwa kukutwa nyumbani kwa Wema na kugundua ni
bangi, kuomba kuvitoa mahakamani hapo kama kielelezo cha ushahidi.
Mulima
kupitia wakili wa Serikali, Costantine Kakula aliomba kuitoa bahasha
iliyofungwa juu yenye muhuri, saini ya shahidi huyo na namba ya maabara
291 ya 2017 ambayo ndani yake kulikuwa na msokoto na vipisi viwili vya
bangi mahakamani hapo kama kielelezo cha ushahidi.
Hata
hivyo wakili wa Wema, Tundu Lissu alipinga kisipokewe kama kielelezo
cha ushahidi kwa sababu ndani ya bahasha hiyo kuna vitu zaidi ya msokoto
mmoja na vipisi viwili vinavyodaiwa kuwa ni bangi.
Kutokana
na hoja hizo, Hakimu Simba alisema Agosti 18, 2017 atatoa uamuzi juu ya
hoja hizo na kesi hiyo pia inaendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa
mashahidi wa upande wa mashtaka.