Kijana Atiwa Mbaroni Kwa Kukutwa na Noti Bandia
Jeshi
la polisi Mkoani Mwanza linamshikilia kijana Fabian Jackson, mkazi wa
Mahina (32) kwa kumkuta na noti 20 za bandia zenye thamani ya shilingi
laki mbili kitendo ambacho ni kosa la jinai.
Taarifa
iliyotolewa na Jeshi la Polisi inasema kwamba polisi wakiwa kwenye
doria na misako walipokea taarifa kwamba katika kijiji cha Kanyara yupo
mtu ambaye ameingia kijijini hapo na ana noti bandia nyingi, baada ya
askari kupokea taarifa hizo walifanya ufuatiliaji wa haraka hadi
kijijini hapo na kufanya upelelezi na msako wa kumtafuta mtu huyo.
Aidha
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza (DCP) Ahmed Msangi ambaye
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo amefafanua kwamba kwa sasa
mtuhumiwa wa tukio hilo yupo kwenye uchunguzi na pindi uchunguzi
utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani na kuongeza kwamba
msako wa kuwatafuta watu wengine wanaoshirikiana na mtuhumiwa huyo
unaendelea ili kuwatia wote mbaroni.
Hata
hivyo Kamanda Msangi amewaonya wananchi wa Mwanza kuacha kutengeneza
noti za bandia kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai na endapo mtu
akikamatwa hatua stahiki za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.