Wema Sepetu abadilishiwa mashtaka katika kesi ya dawa za kulevya
Msanii
wa filamu nchini na Miss Tanzania mwaka 2006, Wema Sepetu jana
alisomewa upya mashtaka katika kesi ya dawa za kulevya inayomkabili yeye
na wenzake pamoja na maelezo ya awali.
Wakili
wa serikali, Constatine Kakula mbele wa Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, Thomas Simba alisema kuwa kesi hiyo ilipangwa
kusikilizwa kwa maelezo ya awali lakini aliomba kufanya mabadiliko
katika hati ya mashtaka, ombi ambalo lilikubaliwa na hakimu hiyo.
Wakisomewa
mashtaka upya, Wema Sepetu na wenzake wanakabiliwa na mashtaka mawili
ambayo ni kukutwa na kiasi kidogo cha dawa za kulevya na kutumia dawa
hizo.
Wakili
wa serikali alidai kuwa Februari 4 mwaka huu katika makazi ya msanii
huyo eneo la Kunduchi, Ununio walikuta msokoto mmoja wa bangi na vipisi
vyenye uzito wa gramu 1.08. Aidha, Wema anatuhumiwa kuwa, Februari Mosi
katika eneo lisilojulikana jijini Dar es Salaam alitumia dawa za kulevya
aina ya bangi.
Watuhumiwa
wakikana mashtaka yote na wakili wa serikali akawasomea maelezo ya
awali. Katika maelezo hayo, wakili huyo anasema baada ya vitu hivyo
kupatikana vilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na kubainika kuwa ni
bangi. Lakini pia Februari 8 Wema alipelekwa kwa mkemia na aligundulika
kutumia bangi.
Wengine
wanaoshtakiwa na Wema Sepetu ni wafanyakazi wake wa ndani, Angelina
Msigwa, Matrida Seleman Abbas ambao nao walikubali sehemu tu ya maelezo
ya awali na kukana shtaka linalowakabili. Katika kesi hiyo, Wema Sepetu
na wenzake wanatetewa na Wakili Peter Kibatala.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 14 mwaka huu.