Rwanda yataka kuchukua sehemu ya anga la Tanzania
Serikali
ya Rwanda imeiliandikia barua Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga
(ICAO) ikitaka kulidhibiti (control) eneo la Kati na Magharibi mwa anga
la Tanzania.
Suala
hilo limekuja wakati Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA)
ikijitahidi kulirejesha eneo la anga la mashariki. Eneo hilo
linalojumuisha Madagascar, Mauritius, Moroni na Kisiwa cha Mayotte
ambalo kwa miaka 39 limekuwa likidhibitiwa na Kenya kutokana na sababu
za kiusalama. ICAO iliipa Kenya eneo hilo ilidhibiti kutokana na
Tanzania haikuwa na rada za ulinzi za kutosha.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye gazeti la THE CITIZEN la
Alhamisi Juni Mosi, 2017, ICAO bado haijaijubu Rwanda ambayo ina rada
mbili za kisasa kwa ajili ya ulinzi wa anga.
Mkurugenzi
Mkuu wa TCAA, Hamza Johari alisema Tanzania kwa sasa inaweza kudhibiti
anga lake lote kwa sababu ipo katika mchakato wa kununua rada nne mpya
zenye thamani ya Tsh 61.3 bilioni.
Rada
hizo zitafungwa katika viwanja vikubwa vitano vya ndege ambavyo ni
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere uliopo Dar es Salaam,
Abeid Amani Karume Zanzibar, Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro, Mwanza na
Songwe.
Mdhibiti
ameweka pia Radio yenye ‘Frequency’ za juu kabisa (VHF Radios) eneo la
Mnyusi Tanga ambazo zimegharimu Tsh 389.9 milioni.
Tumejidhatiti
katika kuhakikisha tunadhibiti eneo letu lote la anga tofauti na sasa
ambapo tunadhibiti asilimia 25 pekee ya anga letu kitu ambacho si
hakikubaliki, alisema Johari.
Kushindwa
kwa Tanzania kudhibiti eneo la kati na magharibi na kuiachia Rwanda,
ina maana kuwa Tanzania itakosa mapato yote yanayotokana na eneo hilo.
Tanzania
imekuwa ikipoteza Tsh 1 bilioni kila mwaka kwa kushindwa kudhibiti eneo
la mashariki ambalo kwa sasa lipo chini ya Kenya.