Mwigulu Nchemba Awataka Chenge, Werema Waeleze Maslahi Yao Mchanga wa Madini
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, ametaka wanasheria wakuu
wa Serikali wastaafu waeleze hadharani maslahi waliyonayo kwenye kampuni
za madini zinazosafirisha mchanga nje ya nchi.
Hatua
hiyo ya waziri imekuja siku chache baada ya wanasheria wakuu wastaafu
waliofanya kazi kwa nyakati tofauti wakati nchi ikiingia kwenye mikataba
ya madini ‘kujivua lawama’ kuhusu udanganyifu uliogunduliwa kuhusa
sakata la usafirishaji wa mchanga.
Wanasheria
hao wakuu wa Serikali wastaafu ni Andrew Chenge na Jaji Frederick
Werema na amewataka wamwache Rais Dk. Magufuli aendelee kulinda
rasilimali za umma zisiliwe na watu wachache.
Mwigulu
amesema hayo juzi, wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara
uliohudhuriwa na mamia ya wananchi wa Tarafa ya Ndago, Jimbo la Iramba.
Alisema
Chenge na Werema kwa nyakati tofauti wakiwa wanasheria wakuu wa
serikali, pamoja na majukumu yao mengine, wameshiriki kusaini mikataba
mikubwa mikubwa, ikiwamo ya makampuni ya kuchimba madini.
“Kwa
akili ya kawaida tu, baadhi ya mikataba mikubwa, ikiwamo ya makampuni
ya madini, haikuwa sawa… ndiyo maana imelalamikiwa kwa muda mrefu.” alifafanua Mwigulu, Mbunge wa Jimbo la Iramba.
Alisema
juzi juzi magazeti yameeleza kuwa akina Chenge na Werema wamedai kuwa
Rais wetu Magufuli amedanganywa na tume maalumu ya Profesa Mruma.
“Wao
ndio waliosaini mikataba ambayo imechangia Taifa kupoteza mabilioni ya
fedha kupitia usafirishaji wa michanga nje ya nchi. Sasa wamegeuka na
kuwa upande wa pili wa watu waliosaini pamoja mikataba hiyo mibovu.
Nawashauri watoke hadharani…. waeleze wana maslahi gani na kampuni
wanazozitetea,” alifafanua zaidi.
Aidha,
Mwigulu amesema Chenge na Werema wakishindwa kuweka wazi maslahi
waliyonayo, basi ni vema wakakaa kimya na kumwacha Rais wa vitendo
aendelee kuinyoosha nchi.
“Hivi
ukimpa mtu kazi ya kuuza duka, halafu kila siku awe anakuambia hajauza
kitu na huku akilalamika kuwa kila siku anapata hasara. Unamshauri
aachane na biashara inayompatia hasara, haachi…anaendelea kuwepo tu,
utamwalewaje. Si atakuwa si mkweli, mwongo ananufaika na hilo duka,” alisema.
Akiijengea
nguvu hoja yake, alisema Chenge na Werema wanaishi Masaki, jijini Dar
es Salaam, hawa hawawezi au watakuwa wamesahau maisha ya Watanzania
wengi maskini waliopo vijijini. Hivyo wamwache Rais Magufuli ambaye
ameonyesha uzalendo wa kweli, aendelee kulinda rasilimali za umma.
Alisema
kwa wao wanaomfahamu Rais Magufuli, kwa hili la kuchokonoa kwenye
madini na kubaini upotevu mkubwa wa fedha za umma, ni mwanzo tu, kazi
bado ipo mbele ya kuchokonoa zaidi ubadhirifu na wizi wa mali ya umma
katika sehemu mbalimbali.
Mwigulu
ametumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania wazalendo wa madhehebu ya dini
mbalimbali waendelee kumwomba Mungu ampe Rais Magufuli afya njema na
ujasiri wa kuziba mwinya yote inayotia hasara Taifa letu.