MJADALA WA BANGI WATIKISA BUNGE,POLISI WATAJWA
Leo wakati mkutano wa saba , kikao cha 40 kikiendela bungeni Dodoma
umeibuka mjadala wa dawa za kulevya aina bangi baada ya baadhi ya
wabunge kusema kuna vitendo vinavyofanywa na baadhi ya polisi nchini
vinatokana na polisi hao kuwa wamelewa bangi.
Katika mjadala huo Mh Spika Job Ndugai naye alichomekea kuwa huwa
anasikia watu wanasema bangi zinaongeza nguvu, hivyo naye alitaka kujua
hizo bangi zinaongeza nguvu za aina gani, huku akiwauliza wabunge ambao
wanatokea maeneo ambayo bangi imekuwa ikiripotiwa sana.
Kufuatia mjadala huo kuendelea alisimama Mbunge Esther Matiko Mbunge wa
Viti Maalumu Mkoa wa Mara na kusema yeye mwenyewe huwa anaona polisi
wakichoma bangi katika maeneo hayo na kudai huenda baadhi ya vitendo
vinavyofanywa na polisi wetu ni kutokana na kuathirika na moshi wa bangi
wakiwa wanachoma bangi hizo. Lakini katika ufafanuzi wa Naibu Waziri wa
Afya alisema polisi hao wao huwa hawaathiriki na moshi huo.
"Jamani tunapojadili juu ya suala la madawa ya kulevya si jambo la
mzaha, ni kwamba polisi wanapokwenda kuchoma bangi mashambani huwa
wanajifunika vifaa maalum lakini hata kama hawajifuniki vifaa hivyo bado
ile bangi ikiingia kwenye miili yao itaondoka ndani ya siku 30 kwani
inageuka na kuwa chumvi na kutoka kwa njia ya mkojo na jasho. Lakini kwa
watu ambao wanatumia kila siku yaani leo, kesho, kesho kutwa na
kuendelea wao wanakuwa ni clonic wa dawa hizo" alisema Kigwangalla
Licha ya Naibu Waziri wa Afya kutoa ufafanuzi juu ya uchomaji wa bangi
lakini Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista
Joakim Mhagama alisimama na kutoa ufafanuzi wake pia akisema kuwa polisi
hawajaathirika na bangi kutokana na namna ambavyo huwa wanachoma bangi
hizo kwa kufuata utaratibu mzuri.
"Mh. Spika vikosi vya polisi vinavyofanya utekeketezaji wa bangi, zipo
njia nyingi wanatumia kuteketeza bangi hizo, kwanza wakiwa wanafanya
zoezi hilo huwa wanaangalia uelekeo wa upepo lakini pia maandalizi
mengine ya vifaa vyao vya uteketezaji wa bangi, aina ya mafuta
yanayotumia kwenye kuchomea bangi hizo vinawafanya kuwa salama kabisa,
kwa hiyo siyo kweli kwamba likitokea tatizo kwenye jeshi la polisi
kwamba polisi wetu wameathirika na matumizi ya bangi, kwani polisi wetu
ni weledi na wanafanya kazi kwa kufuata utaratibu na sheria" alisisitiza
Mhagama
Kwa kumalizia mjadala huo Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema kuwa nchi
nzima na viongozi wamesikia juu ya jambo hilo hivyo wanapaswa kuwa
makini katika utekelezaji wa mambo hayo.