ZIMBWE WA SIMBA APEWA NAFASI YA KUTAMBA TUZO ZA LIGI KUU, NAFASI NYINGINE KWA MAXIME
Hii
leo jioni tuzo mbalimbali za Ligi Kuu Bara msimu wa 2016/17, zitatolewa
baada ya ligi hiyo kufikia tamati wikiendi iliyopita.
Hata
hivyo, Simba inatarajia kutikisa vilivyo safari hii katika tuzo hiyo
tofauti na ilivyokuwa katika misimu iliyopita ambapo ilikuwa ikifunikwa
na Yanga kila wakati.
Tangu
msimu wa 2011/12, mpaka sasa Simba haijawahi kutwaa tuzo ya mchezaji
bora ukilinganisha na Yanga ambayo imechukua tuzo hiyo mara tatu
ikifuatiwa na Azam FC mara mbili.
Kutokana
na hali hiyo, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Mecky Maxime ameliambia
Championi Jumatano kuwa, safari hii Simba inaweza kuchukua tuzo hiyo
kutokana na kuingiza wachezaji wawili katika kinyang’anyiro hicho ambao
ni Shiza Kichuya na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ watakaochuana vilivyo
na Haruna Niyonzima na Simon Msuva wa Yanga, pamoja na Aishi Manula wa
Azam.
Hata
hivyo, Maxime alisema anaamini Tshabalala leo hii ndiye atakayeipatia
Simba tuzo hiyo kutokana na uwezo mkubwa aliounyesha tangu kuanza kwa
msimu huu.
“Nasema
hivyo kwa sababu ndiye mchezaji pekee aliyecheza mechi zote za ligi kuu
bila ya kukosa hata dakika moja, pia amekuwa akitengeneza nafasi nyingi
za kufunga licha ya kucheza nafasi ya ulinzi, hivyo naamini anaweza
kuibuka mchezaji bora hii leo,” alisema Maxime ambaye pia anawania tuzo
ya kocha bora.
Wachezaji
waliyowahi kutwaa tuzo ya mchezaji bora tangu msimu wa 2011/12 mpaka
Msimu wa 2015/16 ni Aggrey Morris (Azam FC), msimu wa 2011/12, Msimu wa
2012/13, alichukua, Kelvin Yondani wa Yanga.
Msimu
wa 2013/14, ilitwaliwa na mshambuliaji wa Azam FC raia wa Ivory Coast,
Kipre Tchetche, 2014/15, aliyechukua tuzo hiyo alikuwa ni kiungo
mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva ambaye kwa sasa pia anawania tuzo
hiyo.
Msimu uliopita wa 2015/16, mchezaji bora alikuwa ni Juma Abdul wa Yanga ambaye msimu huu hayupo kwenye kinyang’anyiro hicho.
Pia
leo tuzo nyingine zitakazotolewa ni ile ya Kocha Bora, Mfungaji Bora,
Mchezaji Bora wa Kigeni, Mwamuzi Bora, Bao Bora na timu yenye nidhamu.