BAADA YA KUTOLEWA AFCON, MANENO YA SERENGETI BOYS KWA WATANZANIA HAYA HAPA
Baada
ya timu ya taifa ya Tanzania chini ya miaka 17, Serengeti Boys kutolewa
katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Vijana, wachezaji wa
timu hiyo wamewaomba radhi Watanzania kutokana na matokeo hayo.
Jumapili
iliyopita, timu hiyo ilikubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Niger
ukiwa ni mchezo wa mwisho wa Kundi B ambapo matokeo hayo yameifanya
Serengeti Boys kumaliza nafasi ya tatu na pointi nne hali iliyosababisha
kutupwa nje ya michuano hiyo.
Kutokana
na kuondoshwa huko, kikosi hicho kinatarajiwa kurejea nchini kesho
Alhamisi kutoka Gabon ambako michuano hiyo ya vijana inafanyika.
Mwenyekiti
wa Maendeleo ya Soka la Vijana Tanzania, Ayubu Nyenzi, amesema: “Tangu
vijana watolewe katika mashindano, wamekuwa hawana raha na wanawaomba
Watanzania wawasamehe kwa matokeo hayo mabaya.
“Tunatarajia
kurejea Tanzania Alhamisi, tumejifunza mengi katika michuano hii hali
ambayo inatufanya tujipange na kutorudia makosa kwenye michuano kama hii
itakayofanyika mwaka 2019 ambapo sisi tutakuwa wenyeji.”