KOCHA ATAKA KIUNGO WA ZAMANI WA YANGA APEWE TUZO NDANDA


Kiungo mshambuliaji wa Ndanda FC ya mkoani Mtwara, Salum Telela huenda akapewa tuzo ya heshima na uongozi wa klabu hiyo kutokana na mchango wake mkubwa alioutoa tangu alipojiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Yanga.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Meja Abdul Mingange ameliambia Championi Jumatano, kuwa jitihada za Telela alizokuwa akizifanya za kuwahamasisha wenzake kupambana kwa nguvu zao zote, ndiyo zimeiwezesha timu hiyo msimu huu kunusurika na balaa la kushuka daraja pamoja na wengine kuonyesha hali ya kugoma.

 “Hali hiyo pia ilisababisha mpaka nikalazimika kuwa nawatumia wachezaji zaidi ya wanne kutoka kikosi cha vijana ili kuziba nafasi za wale waliokuwa wamegoma.
“Kwa kushirikiana na Telela pamoja na wale wachache ambao hawakugoma walipambana na mwisho wa siku tukafanikiwa kuibakiza timu ligi kuu.

“Kusema kweli Telela alikuwa ni mhamasishaji mkubwa kwa wenzake ndani na nje ya uwanja akiwataka kupambana vilivyo ili timu iweze kubakia ligi kuu hivyo kama itawezekana uongozi uangalie jinsi gani ya kumtunuku mchezaji huyo hata kwa tuzo kutokana na mchango wake huo,” alisema Mingange.

SOURCE: CHAMPIONI
Powered by Blogger.