WANAWAKE WANAOJIFUNGULIA NYUMBANI NA NJIANI WATOZWA FAINI YA SHILINGI 50,000/-
BAADHI ya wanawake wa kata ya Lyangalile wilayani Sumbawanga mkoani
Rukwa wamelalamikia kitendo cha kutozwa fedha kiasi cha shilingi 50,000
ikiwa ni adhabu kutokana na kujifungua katika maeneo ambayo siyo salama
na hakuna huduma za uzazi salama.
Wanawake hao walitoa malalamiko yao kwa Katibu wa CCM mkoa wa Rukwa
Mwanamasudi Msafiri Ibrahim Pazi alipokuwa katika kata hiyo akifanya
ziara ya kukagua maendeleo ya chaguzi za ndani ya chama hicho na
kusikiliza changamoto walizonazo wakazi wa kata hiyo.
Wanawake hao walisema wamekuwa wakitozwa fedha hizo na watendaji wa afya
pindi wanapofika katika vituo vya uzazi salama kwa lengo la kupata
matibabu.
Mmoja wa wanawake hao aliyejitambulisha kwa jina la Marystella Kaputa
mkazi wa kata hiyo alisema wanaumia sana kwa kitendo cha kutozwa fedha
hizo kama faini kutokana na kutojifungulia katika eneo ambalo halitoi
huduma za uzazi salama kama majumbani na njiani wanapokuwa wanapelekwa
kujifungua.
Alisema inawezekana nia ni njema ili kuwaadhibu wanawake ambao hawaendi
kujifungua katika vituo vya huduma za uzazi salama lakini adhabu hiyo
imekuwa ni kubwa sana hasa ikizingatiwa kuwa sio wote wanaofanya hivyo
kwa maksudi bali wengine wanajikuta inawatokea kutokana na changamoto
mbalimbali ikiwemo ni pamoja na usafiri, maandalizi duni sambamba na
ndugu zao kutofanya maamuzi wakati uchungu unapo waanza.
Naye Adelina Severino mkazi wa kata hiyo alisema kitendo wanachofanyiwa
wanawake hao sio sawa bali kinachotakiwa ni watendaji wa afya kuendelea
kutoa elimu ili wanawake waone umuhimu wa kwenda kujifungulia katika
maeneo yanayotoa huduma za uzazi salama kama zahanati, vituo vya afya na
hospitali ili kuepuka changamoto zinazoweza kuwakuta wakati
wakijifungua katika maeneo hayo.
Kwa upande wake Sekunde Nanyumbu mkazi wa kata hiyo alisema wakati
mwingine wanawake wanakutwa na hali hiyo kutokana na ndugu wa karibu
kama mume, wakwe na wengine wenye maamuzi katika ukoo kutowaruhusu
ama kufanya maamuzi ya haraka ili wafike katika maeneo yanayotoa huduma
za uzazi salama.
Aliongeza kuwa katika kata hiyo wanategemea zahanati iliyopo katika
kijiji cha Katonto ambapo baadhi yao wanaishi umbali wa kilometa nne
mpaka kuifikia zahanati hiyo hali ambayo imekuwa ikichangia wanawake
kujifungua katika maeneo ambayo siyo salama kwao.
Hata hivyo katibu huyo wa CCM mkoa wa Rukwa alilaani kitendo hicho na
kuahidi malalamiko yao kuyafikisha kwa watendaji wa afya ngazi ya mkoa
ili yashughurikiwe na kukomeshwa kabisa kwani mpaka sasa Sera ya afya
ni huduma bure kwa wakina mama wajawazito kitendo cha kuwa toza faini
siyo sawa.
Kaimu mganga Mkuu wa mkoa wa Rukwa Emmanuel Mtika alikiri kuwepo kwa
malalamiko hayo na kusema kuwa wanaopaswa kupewa adhabu ni wanawake
wanaojifungulia nyumbani na si wale wanao jifungulia njiani lakini pia
tume imeundwa kwa lengo la kuchunguza malalamiko hayo ili hatua ziweze
kuchukuliwa kwani ni kosa kuwatoza faini hiyo ya shilingi 50,000 ambayo
ni kubwa.
Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Sumbawanga